Hali ya kupungua kwa mapigano Hudaida itunzwe.

22 Novemba 2018

Viongozi wa mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa wameonesha kufurahishwa na kupungua kwa mapigano katika mji wa Hudaida lakini pia wakaitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa makundi yote yanayohusika.

Kupitia taarifa ya pamoja iliyotolewa leo mjini New York Marekani, Mark Lowcock Mkuu wa ofisi kuratibu masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto cha UNICEF, Henrietta Fore wamesema “kupungua  kwa mapigano katika mji wa Hudaidah kunaweka hali inayohitajika na maelfu ya raia ambao wamebaki katika mji huo. Tunazisihi pande zote kuitunza hali hii. Wakati huo huo tunaguswa bado na usalama na ulinzi wa raia na miundombinu ya kiraia. Ukatili katika wiki kadhaa zilizopita mjini Hudaida umsababisha uharibifu mkubwa katika sehemu mbalimbali zikiwemo vuto vya afya ambavyo moja kwa moja vimeharibiwa katika mashambulizi au kutwaliwa na makundi yenye silaha”

Wawili hao wameonesha wasiwasi wao kuhusu hospitali ya Al Thawrah ambayo ni ya pekee katika mji huo ambayo ina uwezo wa kutoa huduma za juu, kati na za awali. Lowcock na Fore wamesema hospitali hiyo ni ya muhimu sana kwa mamilioni ya wakazi wa Hudaidah kwani huduma zake ni pamoja na kuhudumia wenye utapiamlo, maeneo mawili ya kuhudumia watu wenye uhitaji wa kuwa chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari na pia inatoa huduma ya dharura ikiwemo kwa watoto wachanga na pi aina kituo cha matibabu kwa wagonjwa wa kipindipindu ambapo watu 1,615 tangu mwezi agosti wametibiwa hapo. Zaidi ya watoto elfu 81 walitibiwa katika hospital hiyo mwaka jana wa 2017 wakati kwa mwaka huu mpaka sasa zaidi ya watu elfu 45 wamepewa matibabu katika hospital hiyo.

“Pande zote zinazohusika katika mgogoro huu tunazikumbusha wajibu wao kufuata sheria na kuzingatia kujali wakati wote kuokoa raia na miundomvinu ikiwa ni pamoja na hospitali ya Al Thawrah na vituovyote vya afya. Na tunatoa wito kwa pande hizo kutochukua au kwa namna nyingine kutumia maeneo ya kiraia kwa shughuli za kijeshi” wameeleza Mark Lowcock na Henrietta Fore.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter