Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana washauriwa kuwa vita havina maana

Kijana mkimbizi kutoka Sudan Kusini. Ni moja wa makabila mengi yaliyoko Uganda.
UNICEF/UN068615/Oatway
Kijana mkimbizi kutoka Sudan Kusini. Ni moja wa makabila mengi yaliyoko Uganda.

Vijana washauriwa kuwa vita havina maana

Amani na Usalama

Tofauti za kikabila, kidini na kijamii ni miongoni mwa  vichocheo vya ghasia katika kambi za wakimbizi nchini Uganda ambako ni hifadhi ya wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Sudan Kusini, Rwanda , Ethiopia na Somalia.

Hiyo ni kwa mujibu wa Kato Sseka Abdu, mratibu na mwanzilishi wa asasi ya kiraia ya “Intergrated Community Development Initiative” inayojihusisha na kuwapa mafunzo vijana wakimbizi hususan  katika kambi  ya Nakivale iliyopo Kusini Magharibi mwa Uganda.

Akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kando mwa mkutano wa 8 wa jukwaa la ustaarabu la umoja huo jijini New York, Marekani, Abdu amesema ni kwa kutambua vyanzo hivyo vya ghasia miongoni mwa wakimbizi ndio maana huwaleta pamoja vijana katika kambi hizo na kuwapatia mafunzo kuhusu umuhimu wa ustaarabu na kuheshimiana huku akifafanua kile mbinu wanazotumia.

“Huwa tunawakusanya kwa kutumia video fulani za matukio mbalimbali kama vile kutoka Palestina na Iraq, na tumekuwa tukitumia kanda kama hizo za video kuwafundisha kuhusu ubaya unaotokana na kujihusisha na visa vya ukreketwa pamoja na ugaidi. Tumeona mabadiliko kwani visa vya ghasia pamoja na ugomvi kati ya vijana wakimbizi vimepungua ndani mwa makazi na pia nje kwa jamii za karibu.”

Abdu amesema amejifunza mengi ambayo atayapeleka  nyumbani ili kuwafundisha vijana.

“..ni kuelewa fika kwamba hakuna haja ya kupigana licha yetu kutoka mataifa tofauti na pia kuwa na mwelekeo tofauti wa kisiasa.”