Mkazi 1 kati ya 2 maeneo ya vijijini huko Amerika ya Kusini ni maskini- FAO

21 Novemba 2018

Umaskini katika maeneo ya vijiijni huko Amerika ya Kusini pamoja na Karibea umeongezeka ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha muongo mmoja, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO katika taarifa yake iliyotolewa leo.

Ikinukuu ripoti mahsusi iliyozinduliwa wakati wa wiki ya kilimo mjini Buenos Aires nchini Argentina, FAO inasema watu wapya maskini milioni mbili wameongezeka kati ya mwaka 2014 na 2016 na hivyo kufanya idadi yao kufikia milioni 59 na hivyo kutishia mafanikio yote ya kuimarisha ustawi wa vijijini kwenye ukanda huo.

“Tangu mwaka 1990 hadi 2014, umaskini vijijini ulipungua kwa asilimia 20 kutoka asilimia 65 hadi 46 lakini sasa kiwango kinaongezeka na idadi ya hohehahe nayo ndio inatia shaka zaidi,” imesema ripoti hiyo ikiongeza kuwa hali hiyo ya mashaka mara ya mwisho kushuhudiwa ilikuwa mwaka 2008 wakati wa janga la kiuchumi duniani.

"Hatuwezi kuvumilia kuona ya kwamba mtu mmoja kati ya wakazi wawili wa vijijini ni maskini. Baya zaidi, tumekumbwa na mrejeo wa hali ya kihistoria ikimaanisha kwamba mwelekeo wetu wa kusonga mbele umebadilika na hivyo ni dhahiri watu wa vijijini wanaachwa nyuma,” amesema Julio Berdegué,  Mwakilishi wa kikanda wa FAO Amerika ya Kusini.

Baadhi ya sababu zilizotajwa kuchochea umaskini vijijini ni hamahama isiyo ya hiari ambapo watu wanalazimika kukimbia maeneo yao kutokana na kukata tamaa, “ukosefu wa usalama, umaskini na hali mbaya ya mazingira,” imesema ripoti hiyo.

Ikifafanua ripoti inasema kuwa mwaka 2015, kipato cha mwaka cha mfanyakazi kijijini kilikuwa dola 363 ilhali kwa mfanyakazi wa mjini kilikuwa dola 804.

FAO inasema kinachotakiwa sasa ni kuondokana na umaskini wa vijijini, hatua ambayo imesema inaweza pia kusaidia kuondokana na shughuli haramu kama vile usafirishaji haramu wa madawa ya kulevya, ukataji magogo kiholela na uchimbaji madini kinyume cha sheria.

Kwa mantiki hiyo ripoti inatoa mapendekezo kadhaa ili kukabiliana na umaskini vijijini huko Amerika ya Kusini ambayo ni pamoja na kuhakikisha sekta ya kilimo ni jumuishi, shirikishi, endelevu na ina tija.

“Pili kuweka mifumo ya hifadhi ya jamii kwa wakazi wa vijijini, tatu usimamizi mzuri wa maliasili pamoja na uendelezaji wa ajira katika sekta zisizo za kilimo vijijini na uimarishaji wa miundombinu.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter