Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamia ya viumbe hatarini kutoweka hatua zisipochukuliwa sasa:UN

Tembo na ndege katika makazi yao ya asili huko Ghana
World Bank/Arne Hoel
Tembo na ndege katika makazi yao ya asili huko Ghana

Mamia ya viumbe hatarini kutoweka hatua zisipochukuliwa sasa:UN

Tabianchi na mazingira

Tathimini iliyofanywa na shirika la kimataifa la muungano wa kupambana na kutoweka kwa aina za viumbe duniani (AZE) imebaini kwamba kuna mamia ya viumbe duniani vitatoweka endapo hatua madhubuti hazitochukuliwa sasa kuvinusuru.

Akiwasilisha tathimini hiyo kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa wa bayo-anuai unaoendelea nchini Misri hadi Novemba 29 mwaka huu , mshirika huyo wa Umoja wa Mataifa ambaye anafanya kazi kubwa ya kubaini , kuchora ramani na kulinda maeneo yanayotambulika kuwa aina za viumbe ambazo ziko hatarini kutoweka , amebaini kwamba karibu nusu ya maeneo ambayo hayatoweza kupatikana tena hayalindwi , lakini kwa kuchukuliwa hatua mujarabu utowekaji wa mamia ya viumbe utaepukwa.

Utafiti huu mpya uliochukuwa miaka mitatu umefanyika kwa ushirikiano wa shirika la kimataifa linaloshughulika na maslahi ya ndege ndege au BirdLife international,Muungano wa kimataifa wa hifadhi ya maliasili (IUCN), hifadhi ya ndege wa aangani ya Marekani (ABC) na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira , UNEP.

Tathimini hiyo mpya imeorodhesha viumbe 1483 vinavijulikana kuwa hatarini katika eneo moja. Pamoja na juhudi za zinazofanyika Chile Muungano wa kupambana na kutoweka kwa viumbe pia una miradi unayoifanyia kazi Brazil na Madagascar, katika nchi hizo tatu miradi inalenga kuimarisha ulinzi wa maeneo yaliyo hatarini, lakini pia kushirikiana kwa karibu na taasisi za fedha ili kujumuisha hifadhi ya viumbe vilivyo hatarini kutoweka katika será zao za kulinda mazingira .

Mratibu wa BirdLife na kiongozi wa maeneo yaliyofanyiwa tathimini hii Dkt. Ian Burfield amesema “tumetambua maeneo 853 ambayo yako hatarini na viumbe vilivyomo ambavyo ni vingi kuliko ilivyodhaniwa hapo awali.Na ili kuokoa kiumbe chcochote kipaumbele cha kwanza ni kulinda makazi yao, lakini asilimia 43 ya makazi hayo hayana mfumo wowote wa ulinzi.”

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la UNEP limesema kutambua na kulinda maeneo hayo yaliyo hatarini ni muhimu sana kwa bayo-anuai na yanafaida kubwa kwa jamii, kuanzia kulinda vyanzo vya maji, kulinda bayo-anuai, kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, na kutoa huduma zingine za asili kwa jamii, kwani maeneo hayo yanauwezekano sio tuu wa kuoa viumbe bali pia kuboresha maisha ya watu.