Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya usalama inatia hofu huku ufadhili ukisusua Cameroon:OHCHR

Familia zikisubiri chakula cha msaada baada ya kurejea Nigeria kutokana na machafuko nchini Cameroon.
UNHCR/Rahima Gambo
Familia zikisubiri chakula cha msaada baada ya kurejea Nigeria kutokana na machafuko nchini Cameroon.

Hali ya usalama inatia hofu huku ufadhili ukisusua Cameroon:OHCHR

Amani na Usalama

Hali ya usalama inayozidi kuzorota katika maeneo mengi nchini Cameroon inatia hofu hususani katika upande wa  kusini magharibi na Kaskazini magharibi huku visa vya utekaji na mauaji vikishamiri imeonya leo ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Ofisi hiyo imesema visa hivyo ambavyo vinatekelezwa na magenge yenye silaha na vikosi vya usalama vinakiuka haki za binadamu na kutozingatia sheria za kimataifa. Akizungumza  na waandishi habari leo mjini Geneva Uswisi, msemaji wa kamishna wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani, amesema kwa zaidi ya mwaka sasa ghasia zimewafanya watu kukosa haki zao za msingi na kuzitaka pande zote kujizuia kuleta ghasia zaidi kwani

“ Mbali na visa vya kuchukua mateka  watoto wa shule 78 na baadaye kuwaachilia huru pamoja na wafanyakazi wa  shule ya sekendari ya Presibetari ya Bamenda katika eneo la  Kaskazini magharibi mapema mwezi huu, kila mara tunapata taarifa za kuwachukua  mateka watu ikidaiwa  kufanywa na makundi yenye silaha yanayataka kujitenga .Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita  tumepokea taarifa za kuchukuliwa mateka  wanafunzi 8 na afisa mmoja wa shule sehemu za Kumba, kusini magharibi na kuwa takribana watawa 13 walichukuliwa mateka  karibu na  Bamessing-Ndop sehemu za kaskazini magharibi. Baadae waliachiliwa huru baada ya wazazi fulani kulipa kikombozi na pia baada ya dayosisi ya kikatoliki ya Kumba kuingilia kati”

Ameongeza kuwa ofisi ya haki za binadamu  inalaani vikali visa vya ukiukaji wa haki za binadamu pamoja na madhila kwa wananchi wa maeneo ambayo yamekumbwa na ghasia na pia kuomba wanaotaka kujitenga kuachana na visa vya matumizi ya nguvu.

Wakati huohuo  Shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura, OCHA, limesema ufadhili wa kusaidia maelfu ya watu nchini Cameroon unasuasua na kwa sasa takriban watu 436,000 hawana makazi kutokana na ghasia hizo. OCHA inasema inahitaji pesa zaidi kuweza kufanikisha shughuli zake kwani ombi la dola milioni 15 ililotolewa mwishoni mwa mwezi Mei kuwahudumia watu 160,000 mpaka sasa imepata  dola milioni 5.

Pia mpango wake wawa jumla wa mwaka 2018 unaohitaji dola milioni 320 kwa kufanikisha msaada wa kibinadamu kwa raia wa Cameroon umefadhiliwa kwa asilimia 37 tu.