Taarifa sahihi za tabianchi zaokoa wakulima na wafugaji nchini Zambia

22 Novemba 2018

Nchini Zambia mradi wa kuwawezesha wakulima na wafugaji kupata taarifa sahihi kuhusu hali ya hewa, umewajengea upya imani baada ya mabadiliko ya tabianchi kuleta misukosuko katika shughuli zao za kilimo na ufugaji. 

Mvua hizo zisizotarajiwa ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi ambayo shuhuda wake pia ni Veneranda Mukume ,mkulima kutoka wilaya ya Gwembe nchini Zambia,“Tangu zamani  tulifahamu kuwa  msimu wa kilimo umewadia. Kulikuwa na viashiria vingi kama vile majani mapya katika miti n.k. Kutokana na alama hizo tulifahamu kuwa sasa ni wakati wa  kwenda mashambani kulima.”

Shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP linasema kuwa wakulima wadogo nchini Zambia walitegemea zaidi mbinu hizo za jadi katika kubaini msimu wa kilimo.

Hata hivyo stadi hizo za kijadi hazihimili mabadiliko ya tabianchi ambapo mafuriko na ukame sasa vimeharibu mazao na mifugo na kuweka hatarini uhakika wa chakula. Mvua kubwa ilinyesha na kusababisha mafuriko na kusomba makazi na mazao yao yote.

Ili kuondoa mkwamo huo, UNDP kwa kushirikiana na serikali ya Zambia na fuko la kusaidia nchi kukabili mabadiliko ya tabianchi, GEF, wameibuka na mradi wa mfumo wa kutoa taarifa kuhusu tabianchi sambamba na maonyo ya mapema sambamba na kupatia stadi wakulima ambapo mratibu wa kilimo wilaya ya Gwembe, Imbuwa Mushemba anasema..

“Kutokana na mradi huo wa taarifa na maonyo, tunawapatia taarifa mapema ambazo zimewawezesha kupanua wigo kutoka zao moja hadi mazao mengi.”

UNDP inasema sasa wakulima katika wilaya za Gwembe, Mambwe na Sesheke wameweza kulima kwa wakati sahihi, kuongeza mavuno na kupata mazao bora ya kupeleka sokoni.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud