Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajabu mtu kuteswa kwa sababu ya kuwa na dini tofauti na wenzake- Guterres

Myazidi kutoka Sinjar  nchini Iraq ambaye alitekwa nyara na kikundi cha ISIL, hapa yuko kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani  ya Mamilyan  huko Akre, nchini Iraq
Giles Clarke/ Getty Images Reportage
Myazidi kutoka Sinjar nchini Iraq ambaye alitekwa nyara na kikundi cha ISIL, hapa yuko kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Mamilyan huko Akre, nchini Iraq

Ajabu mtu kuteswa kwa sababu ya kuwa na dini tofauti na wenzake- Guterres

Haki za binadamu

Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa hii leo kumefanyika mkutano wa 8 wa jukwaa la ustaarabu la Umoja wa Mataifa ambapo Katibu Mkuu Antonio Guterres ameelezea kustaajabu kwake jinsi tofauti ya imani ya kidini na tamaduni vinavyoendelea kuwa chanzo cha mauaji na mateso kwa baadhi ya wakazi wa dunia.

“Hebu msifikirie mbali zaidi ya janga linalokumba waislamu wa kabila la Rohingya huko Myanmar ambao wanakabiliwa na kutokomezwa kwa kabila lao  nyumbani kwao. Au pia wayazidi huko Iraq ambao ISIS wanaua wanaume huku wasichana na wanawake wakitumbukizwa utumwani,” akisema sababu ni wao kuwa tofauti na watesi wao.

Guterres amesema haikubaliki na ni chanzo cha aibu kuwa utambulisho wa mtu au jamii unakuwa sababu ya kulengwa, “ ndio maana ni lazima tufanye kazi pamoja kujenga jamii ambazo zinaheshimiana na jumuishi ambako utofauti unaonekana kuwa ni utajiri na si kitisho.”

 Hata hivyo amesema kushirikiana hakuwezi kufanyika kwa urahisi tu akisema kunahitajika uwekezaji wa utashi wa kisiasa na kujumuisha jamii na viongozi wa kidini.

Katibu Mkuu ametaja mambo matatu muhimu akisema mosi ni mashauriano ya dhati na jumuishi akisema “viongozi wa dini na mashirika ya kidini yana dhima muhimu katika kusongesha maelewano na kupaza sauti za kuondoa mkanganyiko,” akigusia jumuiko hilo la ustaarabu akisema ndio fursa kwa viongozi wa kidini duniani kubadilishana mawazo ya jinsi ya kutekeleza wajibu huo.

Hatua ya pili amesema ni kutumia vema ubunifu na ari ya vijana akipongeza hatua za jumuika la ustaarabu ya kuweka vijana kama kitovu cha shughuli ake.

Warohingya wakivuka mto Naf ili kufikia kambi za wakimbizi nchini Bangladesh
© UNHCR / Andrew McConnell
Warohingya wakivuka mto Naf ili kufikia kambi za wakimbizi nchini Bangladesh

“Kutokana na ongezeko la habari potofu, kauli za chuki kupitia mitandao ya kijamii, vijana wanapaswa kuelimishwa na kujengewa uwezo ili kuondoa mielekeo hiyo potofu,” amesema Bwana Guterres.

Katibu Mkuu ametaja hatua ya tatu kuwa ni kuongeza juhudi kuhakikisha kuwa hatua zote zinaheshimu haki za binadamu kwa mujibu wa tamko la haki za binadamu ambalo mwaka huu linatimiza miaka 70.

“Hii ina maana kuheshimu uhuru wa kuabudu na kujieleza, kusikuwepo na ubaguzi wa aina yoyote na kuheshimu haki ya mtu ya kushiriki na kuhifadhi tamaduni zake,” amesema Katibu Mkuu.

Amerejelea umuhimu wa jukwaa hilo la ustaarabu katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs akisema sasa ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote ule.