Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yakaribisha hukumu ya viongozi wa zamani wa Khmer Rouge

Khieu Samphan(kushoto) na Nuon Chea wakiwa katika mahakama yaCamboadia (ECCC) Picha ya Maktaba
Photo: ECCC
Khieu Samphan(kushoto) na Nuon Chea wakiwa katika mahakama yaCamboadia (ECCC) Picha ya Maktaba

UN yakaribisha hukumu ya viongozi wa zamani wa Khmer Rouge

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Hukumu ya kihistoria iliyopitishwa Ijumaa na mahakama ya kimataifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa dhidi ya viongozi wawili wa zamani wa Khmer Rouge nchini Cambodia kwa makosa ya mauji ya kimbari imekaribishwa na mshauri maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji ya kimbari.

Katika taarifa yake mshauri huyo maalumu Adama Dieng , ameielezea hukumu hiyo ya mahakama ya kimataifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa nchini Cambodia kama ni “siku nzuri kwa haki, ikionyesha kwamba haki ziku zote inashinda na kwamba ukwepaji sharia asilani usikubalike kwa mauaji ya kimari na makosa mengine ya kikatili.”

Nyon Chea ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 92 aliyekuwa kaimu kiongozi wakati wa utawala wa kikatili wa Pol Pot na kiongozi wa zamani wa taifa hilo Khieu Samphan ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 87, walishitakiwa kwa kutokomeza Waislam wa Cham na jamii za Wavietnam wachache, kati ya April 1975 na Januari 1979.

Inaonyesha kwamba haki hushinda siku zote na kwamba ukwepaji sheria asilani usikubalike kwa mauaji ya kimbari na makosa mengine ya kikatili-Mshauri maalumu wa UN , Adama Dieng.

Kitengo maalumu cha mahakama za Cambodia (ECCC) kiliwahukumu wanaume hao wawili kwa kukiuka mkataba wa Geneva wa 1949 na kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu ikiwemo mauaji, kutokomeza, utumwa, kuwasafirisha watu kwa nguvu, kuwafunga, kuwatesa, mauaji ya misingi ya kisiasa, kidini na rangi na kwa vitendo vingine visivyo vya kibinadamu dhidi ya raia nchini Cambodia wakati huo.

Kwa mujibu wa duru za habari hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi yeyote wa Pol Pot wa chama cha kikomunisti cha Kampuchea kilichojulikana kama chama tawala, kuhukumiwa kwa mauaji ya Kimbari.

Katika taarifa nyingine tofauti iliyotolewa na msemaji wake , Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hukumu hiyo inaonyesha kwamba wahusika wa uhalifu wa kikatili kama huo wanaweza kuwajibishwa , hata kama ni miongo mingi baada ya kutekeleza uhalifu huo.

Ndani ya kitengo cha mahakama za Cambodia (ECCC) wakati hukumu ikisomwa katika kesi ya Noun Chea na Khieu Samphan
Picha na :ECCC
Ndani ya kitengo cha mahakama za Cambodia (ECCC) wakati hukumu ikisomwa katika kesi ya Noun Chea na Khieu Samphan

Fikra za Katibu Mkuu ziko na waathirika wa mauaji ya kimbari , uhalifu dhidi ya ubinadamu na ukiukwaji mkubwa wa mikataba ya Geneva ya 1949” amesema Bwana. Guterres katika taarifa yake, na kuongeza kwamba anashukuru kujitoa na kazi kubwa iliyofanywa na kila mtu aliyehusika kwenye kazi ya ECCC na kutoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuendelea kutoa msaada kwa mahakama hiyo.

Bwana.Dieng pia ameelezea mshikamano wake na waathirika, akisema kwamba “watu wote walioteseka kutokana na uhalifu mkubwa uliotekelezwa na Khmer Rouge nchini Cambodia wakati huo wamesubiri kwa muda mrefu kupata haki. Natumai hukumu hii itawafuta majozi”

Amesema pia ni hukumu ya kihistoria linapokuja suala la kuzuia uhalifu kama huo katika siku za usoni.”Wakati uwajibishwaji dhidi ya uhalifu ni nyenzo ya kutoa haki na faraja kwa waathirika, pia unajukumu muhimu la kuzuia kosa lisitokee na kuzisaidia jamii katika juhudi za maridhiano.”

Ameongeza kuwa “Katika wakati huu ambapo tunashuhudia upuuzaji mkubwa na wa hatari wa haki za msingi na viwango vya sheria za kimataifa katika sehemu mbalimbali duniani, hukumu hii inatuma ujumbe mzito katika kanda na duniani kote  kwamba, kwa wale wanaotekeleza, kuchochea au kuunga mkono uhalifu wa kikatili  muda si mrefu watawajibishwa.”