Yemen komesheni vita raia wamechoshwa na adha: WFP

15 Novemba 2018

Wito umetolewa kwa pande zote husika katika mgogoro unaondelea nchini Yemen kukomesha mapigano mara moja ili raia wa kawaida waweze kurejea katika  maisha ya kawaida .

Wito huo wa kusitisha uhasama umetolewa leo mjini Roma Italia na  Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa  la mpango wa chakula duniani WFP, David Beasly, baada ya kukamilisha ziara ya siku tatu ya kikazi  nchini Yemen.

Akielezea baadhi ya aliyoshudia huko, Bw Beasely amesema amesikitishwa na kile alichokishudia hususan katika hospitali ya Hodaydah akisema, ameona , watoto, “ wenye utapiamlo na wamekonda sana na kusalia mifupa mitupu na hawana hata nguvu za kuweza kupumua” . Akaongeza kuwa, “kwa jina la ubinadamu natoa wito kwa pande zote kumaliza vita hivi vibaya. Acheni watoto waishi na watu waanze kujenga upya maisha yao.”

WFP inasema licha ya hali kuzidi kuzorota lakini imeazimia  kuendelea na hata kuzidisha utoaji wa msaada wa chakula na pesa taslimu kwa watu zaidi ya milioni 12 ambao maisha yao yamesambaratika kutokana na vita. Tayari WFP inawahudumia watu kati ya milioni 7 hadi 8 kwa kuwapa chakula kila mwezi.

Mkuu wa WFP amesema  kitu ambacho Yemen inachohitaji wakati huu ni amani kwani ndiyo njia pekee  ya kurejea katika mbinu za kuinua uchumi wake  na kuongeza thamani ya sarafu yake ambayo imeshuka . Lakini vilevile kuanza kuwalipa mshahara wafanya kazi wa umma, ili waweze kupata fedha za kununua chakula na kujikimu kwa mahitaji mengine ya msingi na familia zao.

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter