Baada ya kufanikiwa kufika Rukban, sasa tumepanga misaada zaidi mwezi ujao

15 Novemba 2018

Mshauri mwandamizi wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Jan Egeland amesema kitendo cha misaada ya kibinadamu kuweza kuwafikia wakazi wa Rukban nchini Syria baada ya kushindwa kwa muda mrefu, ni ishara dhahiri ya mafanikio ya diplomasia kupitia utu wa kibinadamu.

Bwana Egeland amesema hayo leo mjini Geneva, Uswisi wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wa kikosi kazi cha usaidizi wa kibinadamu kilichoundwa na kikundi cha kimataifa cha usaidizi kwa Syria, ISSG ambacho kinajumuisha UN, Umoja wa  nchi za kiarabu, Muungano wa Ulaya na mataifa mengine 16.

Mshauri huyo amesema “ Tangu Januari tumejaribu lakini tumeshindwa kufikia eneo hili ambalo limetelekezwa kuliko eneo lolote lile duniani ambako raia wa kawaida kati ya elfu 40 hadi elfu 50 wamekwama kwenye eneo la jangwani karibu na mpaka na Jordan. Kati ya tarehe 3 na 8 Novemba malori 78 yaliweza kufika huko baada ya kupitia moja wa maeneo hatari nchini Syria na kusambaza msaada wa vitu muhimu vya matumizi kama vile , maji, chakula, vifaa vya afya kwa watu wa hapo ambavyo vitawatosha kwa kipindi cha mwezi mmoja.”

WFP ikisambaza chakula cha msaada karibu na Rukban, Syria ambapo msafara wa UN na SARC wa malori 70 kutoka msaada.
WFP
WFP ikisambaza chakula cha msaada karibu na Rukban, Syria ambapo msafara wa UN na SARC wa malori 70 kutoka msaada.

 

Bw Egeland amefafanua kuwa juhudi zao hizo zilifanikiwa baada ya ushirikiano na vikosi vya Urusi vinavyosaidia serikali katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali na pia Marekani kupitia maeneo yanayosimamiwa na makundi sita yaliyojihami.

Akizungumzia usalama wa raia, Bwana Egeland amesema kuwa hali katika kambi wanakoishi raia ni ya kusitisha, wanawake wakiwa katika mazingira magumu zaidi akitolea mfano kisa kimoja..“Kisa kimoja kimesalia kwenye fikra zangu, mama mmoja mwenye  umri wa miaka 13, mama mwenye  umri wa miaka 13 ambaye alipatiwa ujauzito tena. Awali alijifungua katika mazingira ya hovyo. Hakuna hata daktari hata mmoja kwenye kambi hiyo ambaye nafahamu ana ujuzi.”

Kuhusu msaada amesema kuwa watapeleka tena  msafara mwingine wa magari ya msaada huko Rukban kabla ya katikati ya mwezi ujao ili kupeleka vifaa vinavyohitajika haraka kwa sababu majira ya baridi yanakaribia kwenye eneo hilo la jangwani.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter