Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukata watatiza huduma kwa wakimbizi wa Burundi walioko Rwanda

Wakimbizi wa Burundi waliokimbilia kusaka hifadhi nchini Rwanda kufuatia ghasia nchini mwao.
UNHCr/Anthony Karumba
Wakimbizi wa Burundi waliokimbilia kusaka hifadhi nchini Rwanda kufuatia ghasia nchini mwao.

Ukata watatiza huduma kwa wakimbizi wa Burundi walioko Rwanda

Wahamiaji na Wakimbizi

Helena Christensen mmoja wa waungaji mkono wa ngazi ya juu wa shughuli za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR ametoa wito kwa jamii ya kimataifa iwakumbuke na kuwapatia msaada wakimbizi wa Burundi waliopatiwa hifadhi nchini Rwanda. 

Ni sauti ya Helena Christensen, ambaye pia ni mwanamitindo wa siku nyingi kutoka Denmark akisema kuwa yuko kambini Mahama, nchini Rwanda, kambi ambayo ni makazi ya wakimbizi kutoka Burundi na inasimamia na UNHCR.

Anasema kambini hapa amekutana na Alina, mkimbizi kutoka Burundi ambaye akiwa amembeba mwanaye, amemsimulia hali halisi ya maisha  yake..“Tulipowasili hapa, tulikuwa tuna matumaini. Lakini muda mrefu umepita sasa. Ni zaidi ya miaka mitatu na tunapoteza matumaini.”

Ili kufahamu hali halisi ya kambini, mwanamitindo huyu  katika video hii ya UNHCR anaonekana akitembea huku na kule huku akipiga picha na kukutana na watu tofauti akiwemo Paul Kenya mkuu wa kambi hii ya Mahama,“Tulazamika kuchukua uamuzi mgumu hapa kila siku kutokana na ufadhili mdogo mfano je! Tugawe mlo bora? Au tujenge vyoo?? Je turekebishe madarasa ama tununue nguo kwa watoto wachanga? Chochote kile tunachoamua kufanya ama kuacha huathiri maisha ya wakimbizi tunaowahudumia.”

Rwanda inahifadhi wakimbizi 172,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Burundi ambapo asilimia 53 ya wanaotoka Burundi wanaishi kambi ya Mahama na maeneo ya mijini.