Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na Japan kutumia Tokyo 2020 kusongesha SDGs

Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Kimataifa ya UN Alison Smale (kushoto) akiwa na Toshiro Muto, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kamati ya maandalizi ya michezo ya olimpiki itakayofanyika Tokyo 2020, mjini Tokyo
UNIC Tokyo/Takashi Okano
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Kimataifa ya UN Alison Smale (kushoto) akiwa na Toshiro Muto, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kamati ya maandalizi ya michezo ya olimpiki itakayofanyika Tokyo 2020, mjini Tokyo

UN na Japan kutumia Tokyo 2020 kusongesha SDGs

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Umoja wa Mataifa na Kamati ya  Tokyo ya maandalizi ya michezo ya olimpiki  inayohusisha ile ya kawaida na ya watu wenye ulemavu wametiliana saini makubaliano yenye nia ya kusongesha mbele maendeleo endelevu, SDGs kupitia michezo itakayofanyika mjini Tokyo nchini Japan mwaka 2020.

Makubaliano hayo yametiwa saini hii leo mjini Tokyo, Japan na Mkuu wa Idara ya mawasiliano ya Kimataifa ya UN, Alison Smale na Afisa Mtendaji Mkuu wa mashindano hayo ya Tokyo mwaka 2020 Toshiro Muto.

Kupitia makubaliano hayo, pande mbili hizo zimekubaliana kushirikiana ili kusongesha harakati ambazo zitasaidia kuongeza uelewa wa mchango wa michezo na hasa michezo ya olimpiki yam waka 2020 mjini Tokyo katika kufanikisha SDGs hususan miongoni mwa wajapani.

Kamati hiyo na UN zitashirikiana kushawishi matukio ya Umoja wa Mataifa pamoja na majukwaa ya vyombo vya habari ili kuongeza uelewa wa wajapani juu ya  uhusiano kati ya SDGs, michezo na matukio ya michezo miongoni mwa wajapani na raia kutoka mataifa mengine.

“Ninajivunia kutia saini barua hii ya makubaliano, ambayo itaturuhusu kushirikiana na Tokyo 2020 katika kuangazia siyo tu mafanikio ya wanamichezo bali pia ni kwa jinsi gani michezo hiyo inasimamiwa kwa njia bunifu na wajibifu,” amesema Bi. Smale akiongeza kuwa hii ni fursa kubwa ya kutumia majukwaa yetu kuanza majadiliano juu ya mchango wa Tokyo 2020 katika utekelezaji wa SDGs na dhimay a michezo ya olimpiki katika kuendeleza amani na maendeleo duniani.

Kwa upande wake, Bwana Muto amesema, “tangu kuanzishwa kwake, kamati ya maandalizi ya Tokyo 2020 imesisitiza umuhimu wa uendelevu. Kwa kuzingatia dira yay a Tokyo 2020 ya kwamba michezo ina nguvu ya kubadilisha dunia, tumekuwa na mijadala kadhaa kuhusu uhusiano na ushirikiano wetu na UN na tunafurahi sana kutia saini makubaliano haya.”

Amesema kupitia michezo hiyo, wanaweza kusaidia kuongeza uelewa wa masuala ya kimataifa na hatimaye kusaidia kizazi kijacho kuwa jamii endelevu.