Lazima juhudi zaidi zichukuliwe kunusuru bayo-anuai:UN

14 Novemba 2018

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu bayo-anuai unaendelea mjini Sharm El-Sheikh nchini Misri kujadili mbinu za kunusuru bayo-anuai ambayo inazidi kutoweka duniani.

Mkutano huo ulioanza Novemba 13 na kuendelea kwa wiki mbili hadi Novemba 29 , umewaleta pamoja wafanya maamuzi na wawakilishi kutoka nchi zaidi ya 190 kwa lengo la kuchagiza kuongeza juhudi za kulinda bayo-anuai na mfumo mzima wa maisha ya viumbe na mazingira kwa ajili ya uhakika wa chakula, usalama wa maji na afya ya mabilioni ya watu duniani.

Mkutano huo wa Umoja wa Mataifa unafanyika sambamba na mikutano mingine ya bodi na mikataba kuhusu utofauti wa kibaolojia ikiwemo mkutano wa 14 wa pande zilizotia saini mkataba wa bayo-anuai, mkutano wa tisa wa wanachama wa mkataba wa Cartagena juu ya uhasamaji na mkutano wa tatu wa waliotia saini Itifaki ya Nagoya kuhusu upatikanaji na ushirikianaji wa faida.

Katika mkutano huo pia nchi, serikali, mashirika ya biashara, mashirika yasiyo ya kiserikali , miji, watu wa asili, jamii ,vijana na asasi za kiraia, watatoa ahadi za kusaidia mkakati wa utekelezazi wa masuala ya bayo-anuai wa mwaka 2011-220.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter