Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa matokeo ya haraka Mali waleta kicheko kwa wafugaji Gao

Mradi wa matokeo ya haraka (QIP) unaoendeshwa na MINUSMA  nchini Mali umebadili maisha ya wakazi wa mji wa Ansongo mjini Gao ambao awali walitumia mbinu za kijadi kutengeneza mtindi
MINUSMA Video Screenshot
Mradi wa matokeo ya haraka (QIP) unaoendeshwa na MINUSMA nchini Mali umebadili maisha ya wakazi wa mji wa Ansongo mjini Gao ambao awali walitumia mbinu za kijadi kutengeneza mtindi

Mradi wa matokeo ya haraka Mali waleta kicheko kwa wafugaji Gao

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Mali, mradi wa kiwanda cha maziwa uliofadhiliwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini humo MINUSMA umesaidia wafugaji na wazalishaji wa maziwa kuinua siyo tu vipato vyao bali pia kuimarisha uhusiano na utangamano baina yao. Taarifa zaidi na Arnold Kayanda.

Ni katika eneo la Ansongo, lililopo kilometa 90 kutoka mji mkuu wa jimbo la Gao, Gao, ambako wakazi wake licha ya kwamba ni wafugaji na wanalizalisha kiasi kikubwa cha maziwa bado wana tatizo la kipato. Abramane Ibrahim Toure, mkazi wa eneo hili anafafanua..

“Kila wakati tulikuwa na ng’ombe, tuna maziwa, tunakunywa, tunagawia watu, katu hatukuuza maziwa na nikaona bora tushawishi watu tuanze biashara ya maziwa.”

Bwana Toure anasema waliamua kuanzisha kikundi cha wazalishaji maziwa Ansongo, ASPRO-Lait  na kusaka usaidizi kutoka MINUSMA ambayo kupitia ufadhili wa miradi ya matokeo ya haraka ya kuinua kipato cha wananchi na kuimarisha amani ilipatia kikundi hicho dola takribani elfu 45.

Fedha zilitumika kujengea wanachama uwezo wa kusimamia fedha, pamoja na ujenzi wa kiwanda kidogo cha maziwa chenye jokofu na mitambo ya kutenganisha jibini. 

Mohammed Yaya ni mnufaika na anasema “kwa kweli tumefurahi, hapa kuna kiwanda na kina maziwa mazuri na mtu unapata maziwa ya moto na huwezi tena kupata magonjwa.”

Abramane Ibrahim Toure ambaye ndiye mwenyekiti wa ASPRO-Lait anabainisha kwamba, “wanufaika wa kweli si kikundi bali ni wafugaji ambao wameungana na kuanzisha kikundi hiki. Mfano mimi kila usiku naleta lita 10 za maziwa, napata dola 6. Kwa hizo dola 6 nanunua dawa za mifugo iwapo wataugua, nanunua vyakula vya mifugo, na mke wangu anakuwa ana cha kupika kila asubuhi.  Mradi huu umenufaisha sana wafugaji na tunashukuru sana MINUSMA.”