Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko ya tabianchi yanahatarisha amani Sahel-ECOSOC

Familia huko nchini Burkina Faso ikienda kusaka maji. Nchini humo zaidi ya watu 950,000 hawana uhakika wa chakula kutokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha ukame na hivyo kukwamisha shughuli za kilimo na ufugaji.
OCHA/Otto Bakano
Familia huko nchini Burkina Faso ikienda kusaka maji. Nchini humo zaidi ya watu 950,000 hawana uhakika wa chakula kutokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha ukame na hivyo kukwamisha shughuli za kilimo na ufugaji.

Mabadiliko ya tabianchi yanahatarisha amani Sahel-ECOSOC

Tabianchi na mazingira

Baraza la kiuchumi na kijamii la Umoja wa mataifa ECOSOC kwa ushirikiano na kamisheni ya kujenga amani leo limefanya kikao cha kujadili mabadiliko ya tabianchi na uhusiano wake katika kukwamisha juhudi za ujenzi wa amani  na kudumisha amani katika Ukanda wa Sahel.

Akihutubia kikao hicho rais wa ECOSOC Inga Rhonda King amesema ukanda wa Sahel unakabiliwa na chanagmaoto zinazochukua sura mbalimbali akisema “ukosefu wa usalama umesambaa kufuatia mzozo wa makundi yaliyojihami, ukatili na operesheni za kijeshi, madhila kwa binadamu na mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka kila uchao.Watu milioni 4.9 wamefurushwa makwao mwaka huu huku watu milioni 24 wakihitaji msaada wa kibindamu katika ukanda mzima.”

Bi. Rhonda amesema ukanda huo ni moja ya maeneo yaliyoathirika zaidi kimazingira duniani huku viwango vya joto vikitabiriwa kuwa mara 1.5 zaidi ya viwango vya dunia nzima.

Ameongeza kuwa , ukanda huo unategemea kwa kiasi kikubwa kilimo cha mvua na hukabiliwa mara kwa mara ni kiangazi na mafuriko na kusababisha athari kubwa kwa usalama wa chakula.Tunapozungumza watu takriban milioni 33 hawana uhakika wa chakula wakati watoto milioni 4.7 walio na umri wa chini ya miaka mitano wanakabiliwa na utapiamlo uliokithiri.”

Rais huyo wa ECOSOC ameongeza kuwa wakati idadi ya watu ikitarajiwa kuongezeka kwa asilimia 2.8 kila mwaka katika mazingira ambamo rasilimali zinapungua, ikiwemo ardhi na raslimali maji, mabadiliko ya tabianchi katika ukanda wa Sahel yanaweza kuchochea hatari.

Inga Rhonda King, Rais wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa
UN /Rick Bajornas
Inga Rhonda King, Rais wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa

Amesema“hatari ambazo zinaweza kuzua mizozo na kulazimisha watu kuhama, changamoto ambazo zinakumba uakanda huo.Hali hii inahitaji kushughulikiwa haraka.”

Akizungumzia athari za mabadiliko ya tabianchi katika kuchochea mizozo wiki hii Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, “ili kupata amani na maendeleo endelevu na kutoka katika uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu na kupunguza na kumaliza mahitaji ya kibindamu, ni lazima tutatue miziz ya mizozo na majanga. Hii inapatikana katika ubaguzi, ukiukwaji wa haki za bindamu, utawala dhaifu, mizozo na athari za mabadiliko ya tabianchi’.

Kwa upande wake Mwenyekiti ya kamisheni ya kujenga amani Ion Jinga amesema, mabadiliko ya tabianchi yanaathiri dunia nzima na kusababisha ikiwemo, majangwa, ukame , mafuriko na ukosefu wa chakula vyote vikihatarisha vizazi na maendeleo.”

Ameongeza kuwa ECOSOC kwa ushirikiano na kamisheni yake zinaweza kusaidia miradi mashinani kwa kuambatanisha sera, kujenga ushirikiano na kuwekeza raslimali na kuchagiza umiliki wa kitaifa miradi inayowekezwa.

Kikao hicho kilijadili pia namna Umoja wa Mataifa utaimarisha mifumo kwa ajili ya kusaidia nchi za ukanda wa Sahel katika kuimarisha ustahimili wake dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Ukosefu wa usalama na ukame vimesababisha njaa ukanda wa Sahel na kulazima mashirika ya Umoja wa Mataifa kama WFP kulazimika kugawa mlo kwa wakazi wa eneo hilo.
WFP/Sébastien Rieussec
Ukosefu wa usalama na ukame vimesababisha njaa ukanda wa Sahel na kulazima mashirika ya Umoja wa Mataifa kama WFP kulazimika kugawa mlo kwa wakazi wa eneo hilo.