Kuwarejesha wakimbizi wa Rohingya Myanmar ni kuwatosa katika mzunguko wa ukatili-Bachelet

13 Novemba 2018

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet ameitolea wito serikali ya Bangladesh kusitisha mipango ya kuwarejesha wakimbizi wa Rohingya Myanmar akionya kuwa urejeshaji huo huenda ukakiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu na kuyaweka maisha yao na uhuru wao hatarini.

Kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya haki za binadamu, inaendelea kupokea taarifa za ukiukwaji wa haki za Warohingya walioko Kaskazini mwa jimbo la Rakhine ikiwemo madai ya mauaji, kutoweka, kukamatwa kiholela na ukandamizaji wa haki na uhuru wa kutembea, afya na elimu.

Aidha watu takriban 130,000 ni wakimbizi wa ndani huku idadi kubwa ni wa kabila la Rohingya ambao wengi wanasalia kambini ambako haki zao zinakandamizwa ikiwemo haki ya utaifa.

 Bi. Bachelet amesema, “tunashuhudia hofu na woga miongoni mwa wakimbizi wa Rohingya walioko Cox’s Bazar ambao wako hatarini kurejeshwa Myanmar bila hiari yao.” Ameongeza kuwa, “Kuwarejesha kwa nguvu wakimbizi na waomba hifadhi nchini mwao ni ukiukwaji wa sheria ya kimataifa inayozuia urejeshwaji wa nguvu iwapo kuna hatari ya kuteswa au dhidi ya uhai na usalama wa mtu.

Yaelezwa kuwa baadhi ya wakimbizi wametishia kujiua iwapo watarejeshwa kwa nguvu ambapo tayari wanaume wawili walioko Cox’s Bazar wamejaribu kujiua.

Mkimbizi wa Rohingya, Tahara Begum, akiwa na mtoto wake katika kambi ya Kutupalong, Coxs Bazar, Bangladesh
UNHCR/David Azia
Mkimbizi wa Rohingya, Tahara Begum, akiwa na mtoto wake katika kambi ya Kutupalong, Coxs Bazar, Bangladesh

 

Bachelet ameitolea wito serikali ya Myanmar kuonyesha u tayari wake kuweka mazingira ambayo yatawawezesha wa Rohingya kurejea kwa kutatua mizizi ya janga la jimbo la Rakhine na ubaguzi dhidi ya waRohingya.

 Kwa upande mwingine ameisihi serikali ya Bangladesh ihakikishe kwamba urejeshwaji unaambatana na viwango vya kimataifa vya kurejea kwa hiari, wenye hadhi, salama na uwazi na pale mazingira yanaruhusu.

Ofisi ya haki za bianadamu imesema ukatili dhidi ya Warohingya ni mbaya zaidi ikiwemo uhalifu dhidi ya utu na hata mauaji ya kimbari bila ya uwajibishwaji wowote amabpo kuwarejesha wakimbizi wa Rohingya Myanmar ni kuwatosa katika mzunguko wa ukatili ambao jamii hii imeshuhudia kwa karne.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter