Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yajizatiti kusaidia Wayemen licha ya changamoto

Bandari ya Hudeidah katika Yemen ni moja wa bandari inayosadia watu wa huko kwa kushughulikia misaada ya kibinadamu pamoja na mafuta.
UNICEF/Abdulhaleem
Bandari ya Hudeidah katika Yemen ni moja wa bandari inayosadia watu wa huko kwa kushughulikia misaada ya kibinadamu pamoja na mafuta.

UN yajizatiti kusaidia Wayemen licha ya changamoto

Amani na Usalama

Mapigano makali yanaendelea kuongezeka kwenye sehemu mbalimbali za mji wa bandari wa Hodeidah katika kipindi cha saa 72 na kushuhudiwa pia karibu na hospitali ya Al-Thowra moja ya hospitali kuu za jimbo hilo ambako watoto wawili na muuguzi mmoja wamejeruhiwa baada ya risasi kupenya katika kitengo cha dharura cha watoto.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi msemaji wa Shirika la afya ulimwenguni, WHO, Christian Lindmeier amesema kuchachamaa kwa mzozo kumezuia watu kupata huduma muhimu za afya Hodeidah huku idadi ya wagonjwa na wanaosaka matibabu kila siku ikipungua katika hospitali ya Al-Thawra.

Bwana Lindmeier amesema WHO wiki iliyopita iliwasilisha lita 127,000 za petroli kwa hospitali za Al-Thawra, Al-Salakhana na Al-Salam pia kutoa  mifuko 2,000 ya kuhifadhi damu.

Wakati huohuo Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limesema licha ya mashambulizi katika siku za hivi majuzi lakini maghala ya msalaba mwekundu hayajaharibiwa na hakuna uharibifu wowote wa tani 51,000 za ngano ambazo ni lishe kwa takriban watu milioni 3.7 Kaskazini na kati kati mwa Yemen katika kipindi cha mwezi mmoja.

Kwa mujibu wa msemaji wa WFP Herve Verhoosel akizungumza na waandishi wa habari Geneva Uswisi “Katika siku chache zilizopita mashine za kusaga zinasimamiwa na muungano ambapo WFP inahitaji kufikia mashine hizo haraka iwezekanavyo ili kuweza kuendesha shughuli zake.”

WFP haijaweza kutumia kiwanda cha kusaga unga tangu mwezi Agosti kwa sababu ya mapigano, Mkurugenzi Mkuu wa WFP yuko Yemen tangu Jumatatu kwa ajili ya kutathmini uhakika wa chakula na kufanya kazi na timu nchini humo na wadua wengine kwa ajili ya kuweza kufikia watu wengi zaidi walio na mahitaji. Licha ya hali ngumu, WFP inasaidia watu milioni 8 kwa kuwapa chakula na vocha za chakula.