Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko yakiendelea Gaza UN yahaha kurejesha utulivu.

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu kwa ajili ya eneo linalokaliwa la Wapalestina, Jamie McGoldrick ametewatembela wagonjwa katika hospitali ya Al-Shifa mjini Gaza.
UNRWA/Khalil Adwan
Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu kwa ajili ya eneo linalokaliwa la Wapalestina, Jamie McGoldrick ametewatembela wagonjwa katika hospitali ya Al-Shifa mjini Gaza.

Machafuko yakiendelea Gaza UN yahaha kurejesha utulivu.

Amani na Usalama

Wakati machafuko yakiendelea kushika kasi upya kwenye Ukanda wa Gaza , Umoja wa Mataifa unasema unafuatilia haki kwa karibu huku mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa kwenye ukanda huo Nickolay Mladenov akishirikiana na pande zote kujaribu kurejesha utulivu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Bwana Mladenov wamezitaka pande zote kukomesha machafuko huku duru zikisema kwamba msako, mabomu kutoka vikosi vya Israel na maroketi yanayovurumishwa na Palestina yamaekatili maisha ra watu wasio na hatia.

Duru hizo zinasema machafuko haya mapya yamezuka Jumapili jioni wakati wakati wa operesheni ya vikosi maalumu vya Israel maili kadhaa kwenye Ukanda wa Gaza na kusababisha vifo vya Wapalestina sita.

Wakati ghasia hizo zikiendelea upungufu mkubwa wa vifaa na uwezo kuendesha hospitali ya Shifa ambayo ndio hospitali kubwa Gaza kunawanyima wagonjwa fursa ya kurejea katika maisha ya kawaida au hata kuweza kuinuka na kutembea tena na kuongeza muda wao wa kupona miaka mitatu au hata minne.

Madaktari katika hospitali hiyo wameelezea kuchanganyikiwa kwa sababu ya hali hii, huku mmoja wao akiiambia UN News kuwa anatamani asingekuwa daktari kwa sababu ya kushindwa kutibu wagonjwa wake kutokana na ukosefu wa dawa na zana za kufanyia kazi.

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu kwa ajili ya eneo linalokaliwa la Wapalestina, Jamie McGoldrick amezuru hospitali hiyo na kuzungumza na wagonjwa mbalimbali na madaktari

“Sekta ya afya Gaza imekuwa katika upungufu mkubwa wa ufadhili kwa miaka. Vikwazo vya Israel kwa miaka 12 vimezuia kuingia kwa bidhaa na watu kutembea hali ambayo imesababisha ukosefu wa nadawa muhimu.” Jamie amesema.

McGoldrick ameongeza kuwa watu takriban 20,000 wamejeruhiwa katika maandamano waliyoyaiita “Maandamano ya marejeo”mjini Gaza  huku wengi wakiwa wamepigwa risasi miguuni,

"Tulichoshuhudia hospitali ni mamia ya vijana wa kiume na wanawake wanaohitaji operesheni 6 au 7 za kurekebisha mifupa ambazo zinaweza kuchukua miaka miwili na kugharimu mamilioni ya dola na pia wanahitaji msaada wa kiufundi na rasilimali zingine ambazo hospitali hii au Gaza hazina.”

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu kwa ajili ya eneo linalokaliwa la Wapalestina, Jamie McGoldrick alipotembelea hospitali ya Al-Shifa mjini Gaza.
UNRWA/Khalil Adwan
Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu kwa ajili ya eneo linalokaliwa la Wapalestina, Jamie McGoldrick alipotembelea hospitali ya Al-Shifa mjini Gaza.

 

Kwa sababu ya ongezeko hilo la majeruhi hospitali ya Shifa  imelazimika kuahirisha operesheni karibu 8000 kwa wagonjwa wa saratani, moyo na magonjwa mengine.

Mahmoud, mwenye umri wa miaka 29, mmiliki wa duka mjini Gaza anaugua hospitalini Shifa kwa sababu alijeruhiwa wakati akishiriki maandamano

“Nilijeruhiwa kwa risasi wakati nikishiriki maandamano , hali yangu ya kiafa ni mbaya , nilipoteza sehemu ya mifupa kwenye mguu na madaktari wanasema matibabu yangu yatachukua kati ya miaka 3 na 4.”

Hassan Hanneya, naye mwenye umri wa miaka 32, alijeruhiwa pia kwenye maandamano anamatumaini kwamba ipo siku vizuizi vya Isarel vitaondolewa na watu wa Gaza kuwa na maisha ya kiutu.

"Nilipigwa risasi kwenye mishipa ya ateri , nyingine kwenye veini , kwenye neva na nyingine kwenye mifupa. Mfupa wangu ulipasuka sentimita 15. Majeraha yangu ni mabaya sana na madaktari wanajaribu kunipa rufaa kwenda hospitali nje ya Gaza lakini bado nasubiri.”

Dr. Mahmoud Mattar, ni miongoni mwa madakrati wa ngazi ya juu katika hospitali ya Al-Shifa anazungumzia upungufu wa vitendea kazi ni moja ya vitu vinavyomuhuzunisha sana

“Uwezo wa huduma za msingi baada ya vizuizi vya miaka 12 unakwisha hivyo waweza kufikiria hali ikoje linapokuja suala la vitendea kazi vinavyohitajika kutibu mifupa iliyovunjika . Ni shida kugawanya vifaa vichache tulivyonavyo kwa wagonjwa wote hivyo wengine hatuwezi kuwafanyia chochocte. Endapo tuaweza kuokoa mguu na kuzuia usikatwe, majeraha mara nyingi huishia kuwa ulemavu wa kudumu.”

Dkt. Mattar amesisitiza kwamba haja ya kukomesha umwagaji damu na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuzisaidia hospitali za Gaza na kutoa msaada wa yale wanayohitaji kukabiliana na idadi kubwa ya wajeruhi ambayo imezidi uwezo wa hospitali za Gaza.

Mkurigenzi wa hospitali ya Al-Shifa Dkt. Medhat Abbas akizungumzia changamoto nyingi katika hospitali hiyo amesema kwa miaka 30 aliyofanya kazi katika masuala ya udaktari hhajawahi kushuhudia hospitali inashindwa kutoa hata chakula kwa wagonjwa wake huduma ambayo ni muhimu katiika safari ya kupona kwa wagonjwa. 

Pia amresema wagonjwa wengi katika Hospitali ya Shifa wanalala kwenye ushoroba usiku kwa sababu hospitali imefurika na vitanda pia havitoshi.

"Tangu mwezi May hospital za Gaza zimeshindwa kutoa huduma ya chakula kwa wagonjwa wake na pia kuna upungufu mkubwa wa madawa , mishahara, vifaa vya tiba , vifaa vya ukarabati na vitanda kwa ajili ya wagonjwa.Kila siku kuna wagonjwa ambao wanalazimika kulala kwenye ushoroba kwa sababu vyumba havitoshi . Vilevile kuhimili idadi kubwa ya watu wanaojitolea, kwa sababu hatuwezi kuwalipa gharama za usafiri kufika hospital.Kuna mgogoro wa mishahara pia ambao unaathiri wafanyakazi wa Gaza na mamlaka ya wafanyakazi wa Palestina Gaza , baadhi ya watu wanalipwa asilimi 40 tu ya mishahara yao na wengine asilimia 50.”

Mtoto wa umri wa miaka 12 akipita pembezoni mwa nyumba iliyobomolewa na mashambulizi kutoka angani yaliyofanywa na Israeli katika jiji la Rafah, kusini mwa Gaza mwaka 2012.
UNICEF/UNI132737/El Baba
Mtoto wa umri wa miaka 12 akipita pembezoni mwa nyumba iliyobomolewa na mashambulizi kutoka angani yaliyofanywa na Israeli katika jiji la Rafah, kusini mwa Gaza mwaka 2012.

 

Naye Dkt. Mohammed Dhaher tmwakilishi wa shirika la afya duniani, WHO Gaza amesema Zaidi ya asilimia 50 ya visa vya kitabibu vinavyohitaji rufaaa havipatiwi vibali vya lazima vinavyohitajika.

“Ukanda wa Gaza unakabiliwa na kipindi kigumu sana , kwa Zaidi ya miaka 10 ambayo inajumuisha vizuizi vya Israel, kuzorota kwa hali ya huduma za kijamii, kuongezeka kwa umasikini, na ukosefu wa ajira. Kila mwaka Zaidi ya watu 24,000 wanaomba vibali vya vya kwenda kupata matibabu nje kutokana ukosefu wa uwezo kwenye hospitali za Gaza.”

Kesi nyingi za wagonjwa hao hupewa rufaa kwenda hospitali za Jerusalem, Jordan na Misri. Na kutokana na vikwazo vya Israel Jamei McGoldrick amesema wagonjwa wengi hawana njia bali kusaka huduma ndani ya Ukanda wa Gaza.Ankiongeza kuwa “ Huwezi kwenda popote, watu wamekwama hapa , wanalazimika kusaka matibabu hapa Hivyo ni lazima tuboreshe uwezo wa hospitali kuweza kutibu wagonjwa hawa na kuwapa watu fursa ya kuishi Maisha bora. Na hili linahitaji fedha, msaada na ahadi lakini kwa bahati mbaya hivi sasa hatuoni hili kuwa endelevu.”

Amesema suluhu pekee anayoiona ni ya kisiasa , lakini hadi hapo itakapotimia ameomba jumuiya ya wahisani kuongeza msaada wake ili kuokoa Maisha ya mamilioni ya watu wa Gaza.