Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa amani DRC ni kidonda moyoni mwangu-mkimbizi Lubunga

Aliyekuwa mkimbizi kutoka DRC, Lubunga Mwendanababo, sasa ni raia wa Marekani.
UN News/Assumpta Massoi
Aliyekuwa mkimbizi kutoka DRC, Lubunga Mwendanababo, sasa ni raia wa Marekani.

Ukosefu wa amani DRC ni kidonda moyoni mwangu-mkimbizi Lubunga

Wahamiaji na Wakimbizi

Mpango wa shirika la wakimbizi duniani, UNHCR wa kuwapatia wakimbizi walioko Tanzania hifadih katika nchi ya tatu umeendelea kuleta tija kwa wakimbizi wakiwemo wale kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambao sasa wanapazia jinsi walivyonufaika. 

Hii ni sauti ya Lubunga mwendanababo, mkimbizi kutoka DRC, ambaye aliishi katika kambi ya Nyargusu nchini Tanzania.

Kijana huyu ambaye alikimbia DRC miaka ya tisini akiwa na umri wa miaka mitano katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa anakumbuka maisha yake kambini.

“Tuliingia kwenye boti tukaenda mapka Tanzania, tukaishi pale tulikuwa tunalala kwenye hema, baada ya pale tukajenga nyumba ya matofali, chakula tulikuwa tunapokea pale ila kuni tulikuwa tunatafuta wenyewe na tulipofika walitupatia nguo na viatu.”

Mzawa huyu wa DRC licha ya kwamba sasa yuko Marekani ambapo amemaliza shahada ya kwanza na sasa anafanya kazi bado analilia nchi yake.

“Inasikitisha sana na moyo wangu unauma, kwa sababu mimi ni mkongomani ninapoangalia habari kwamba kuna watu wameuwawa, watoto wanatumikiswah jeshini, wanawake wanabakwa, inaniumiza sana lakini ninaimani kuwa DRC itapata amani.”

 

 Sasa hivi Mwendanababo ana ndoto za kusoma hadi shahada ya uzamili na anasema elimu imekuwa msingi muhimu katika maisha yake.

“Nilikuwa na matumaini ya kuwa kutakuwa na maisha baada ya vita na sikukata tamaa, niliamini kuwa shule ni msingi wa maisha na wazazi wangu kwa kuwa wamesoma walinisukuma kuendelea na masomo licha ya kuwa ukimbizini.” 

Hata hivyo ukosefu wa amani DRC bado ni kidonda moyoni-mkimbizi Lubunga.