Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sekta ya ubunifu wa nguo nayo yahaha kulinda mazingira

Mbunifu wa mitindo ya nguo  Lara Khaoury akiwa katika studio mjini Beirut.
UN Women/Joe Saade
Mbunifu wa mitindo ya nguo Lara Khaoury akiwa katika studio mjini Beirut.

Sekta ya ubunifu wa nguo nayo yahaha kulinda mazingira

Tabianchi na mazingira

Wakati dunia ikihaha kusaka mbinu za kukabiliana na uchafuzi wa mazingira, sekta ya ubunifu wa mitindo nayo imeshachukua hatua ili kuhakikisha bidhaa zake haziharibu mazingira.

Makala iliyochapishwa na shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP inataja viwanda vya nguo kuwa vinazalisha asilimia 20 ya majitaka na asilimia 10 ya hewa chafuzi.

“Kila sekunde, malapulapu ya mabaki ya viwanda vya nguo yenye ujazo wa sawa na lori moja hutupwa kwenye madampo ya taka au huchomwa moto. Iwapo hakuna mabadiliko kwenye kitendo hiki, ifikapo mwaka 2050, sekta ya viwanda vya nguo itakuwa imetumia karibu robo kiwango cha hewa ya ukaa kinachovumilika duniani,” imesema UNEP.

Kama hiyo haitoshi, shirika hilo linasema ufuaji wa nguo nao husababisha tani nusu milioni za nyuzi ndogo ndogo za vitambaa kuingia kwenye bahari kila mwaka.

Sambamba na uharibifu wa mazingira, makala hiyo inataja pia gharama za kijamii ambapo wafanyakazi katika sekta ya nguo, “hulipwa ujira mdogo sana na kulazimika kufanya kazi kwa muda mrefu na katika mazingira duni.

Hata hivyo UNEP inasema kutokana na kilio cha walaji, tayari hatua zimeanza kuchukuliwa kurekebisha  hali hiyo wakati huu ambapo shirika hilo linajiandaa kwa mkutano wa Baraza lake mwezi Machi mwakani.

Patsy Perry ambaye ni mhadhiri mwandamizi wa masuala ya ubunifu wa mitindo katika Chuo Kikuu cha Manchester anasema “wauzaji rejareja wa nguo hivi sasa wanafikia kuhusu suala la uendeleveu kwenye sekta hii na wanajaribu kubuni mbinu za kuhakikisha sekta ya nguo haichafui mazingira.”

Kampuni ya Ecoalf ya Hispania ambayo inatengeneza viatu kutokana na mimea aina ya mwani na pamoja na kutumia taka za plastiki zinazookotwa kutoka katika bandari 33 na kuzigeuza kuwa viatu, mabegi na nguo.

Nyingine ni Patagonia, ya California nchini Marekani ambayo imekuwa ikitengeneza makoti kwa kutumia chupa zilizotupwa.

Nayo kampuni ya H& M imeibuka na kampeni yake ambapo mtu akirejesha kiasi fulani cha nguo au viatu asivyovihitaji, anapatiwa punguzo la bei pindi anaponunua vitu vingine.

Hata hivyo amesema bado kuna tatizo kwa kuwa muundo wa biashara ya nguo ni wa kasi ambapo mapato yanatokana na kiwango cha mauzo, kwa hiyo ni lazima wafanyabiashara wa rejareja waibuke na mitindo mipya kila wakati.

“Litakuwa si jambo la halisia kutajarajia wanunuzi waache kununua nguo kwa kiasi kikubwa, kwa hiyo kwa kuelekea mbele, natarajia kuona ubunifu zaidi wa mbinu za kisasa endelevu za uzalishaji, matumizi ya rangi bila maji na suluhu bunifu za utupaji wa taka za sekta  hii ya viwanda vya nguo,” amesema Bi. Perry.

Kauli mbiu ya mkutano huo wa Nne wa Baraza la UNEP, ni Fikiria zaidi ya mwenendo wa sasa na ishi kiendelevu, ujumbe ambao unaenda sambamba azma ya wabunifu wa mitindo na wauza nguo rejareja ya kurekebisha sekta hiyo ya nguo.

UNEP inasema ni katika mkutano huo ambapo watazindua rasmi Ushirika wa UN kwa sekta endelevu ya ubunifu wa mitindo ili kuhamasisha sekta binafsi, serikali, mashirika ya kiraia kuweka shinikizo kubwa zaidi la kupunguza athari hasi za kijamii, kiuchumi na kimazingira zitokanazo na sekta hiyo ili hatimaye iwe kichocheo cha kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.