Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Komesheni mauaji ya raia Yemen- Bachelet

Mapigano makali katika mji wa bndari wa Hudeidah yanakaribia  hospitali ya Al Thawra
© UNICEF/UN0253576/Abdulhaleem
Mapigano makali katika mji wa bndari wa Hudeidah yanakaribia hospitali ya Al Thawra

Komesheni mauaji ya raia Yemen- Bachelet

Amani na Usalama

Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa  Michelle Bachelet ameeleza kuchukizwa kwake na ukatili unaoendelea katika mji wa bandari wa Hudaidah, vitendo ambavyo amesema tayari vimesababisha madhila kwa wananchi wengi wa Yemen.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopokelewa na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, takriban mashambulio ya angani110 yamefanywa dhidi ya miji ya Hudaidah, Sa’ada na Sana’a kati ya Oktoba 31 na Novemba 6 na mashambulio yameongezekatangu wakati huo.

Ofisi hiyo imetoa taarifa hii leo ikimnukuu Bi Bachelet akisema kuwa vikosi vya ushirika ambao unaongozwa na Saudi Arabia pamoja na vikosi vinavyounga mkono wahouthi na pia wale wote wanaounga upande mmoja au mwingine kwa kuwapatia silaha ama msaada wowote ule katika mgogoro huo wachukue hatua za haraka kukomesha mateso kwa raia wa kawaida wa Yemen.

Mji wa Sana'a Yemen ulikuwa ukionekana mwaka wa 2015
OCHA/Charlotte Cans
Mji wa Sana'a Yemen ulikuwa ukionekana mwaka wa 2015

 

Amesema ukiukwaji wowote ule unaofanywa na upande mmoja katika mgogoro huo si idhini kwa upande mwingine kujibiza kisasi kwa gharama yoyote ile  kwani hata vita husimamiwa kwa kanuni na pande zote katika mgogoro huo zinawajibika  kuheshimu sheria za kibinadamu za kimataifa na sheria za haki za binadamu zinazotumika.

Inaelezwa kuwa ndege za kivita  za ushirika  zimekuwa zikipaa kwa umbali mdogo kutoka ardhini kwenye anga ya mji wa Hudaidahtangu Alhamisi asubuhi huku vikosi vya wahouthi vikijibu mashambulizi kwa kufyatua mizinga yakutungua ndege na silaha zingine nzito.

Vijana wa kiume wakiwa wamesimama katika jengo lililobomolewa sehemu za Saada,Yemen
WFP/Jonathan Dumont
Vijana wa kiume wakiwa wamesimama katika jengo lililobomolewa sehemu za Saada,Yemen

 

Takriban raia  23 wamethibitishwa kufariki dunia mjini Hudaidah tangu tarehe 24 mwezi uliopita wa Oktoba, ingawa idadi kamili inaweza kuwa kubwa zaidi ya hiyo.

Halikadhalika watu 445,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani mjini Hudaidah tangu mwezi Juni mwaka huu wa 2018.