Shambulio lingine leo Mogadishu, UN yalaani vikali

9 Novemba 2018

Umoja wa Mataifa umelaani vikali mashambulio ya bomu yaliyotokea hii leo kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na kusababisha vifo vya watu na majeruhi.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, magari matatu yaliyokuwa na vilipuzi yalilipuliwa karibu na hoteli ya Sahafi leo mchana, matukio ambayo yalifuatiwa na watu wenye silaha kufanya mashambulizi.

Magaidi wa Al Shabaab wamedai kuhusika na mashambulio hayo ambayo kwa mujibu wa vyombo vya habari  yamesababisha vifo vya watu 20 na makumi kadhaa wamejeruhiwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake mjini New York, Marekani, amelaani mashambulizi hayo akituma rambirambi kwa familia za wafiwa huku akiwatajia ahueni ya haraka majeruhi.

“Naamini kuwa wasomali katu hawatokatishwa tamaa na ghasia za aina hiyo na wataendelea na harakati zao za kusaka mustakabali wenye ustawi,” amesema Bwana Guterres.

Amesisitiza usaidizi na mshikamano na wananchi wa Somalia katika kufanikishi harakati hizo.

Wakati huo huo, Naibu Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM Raisedon Zenenga amesema nao pia wanalaani mashambulizi hayo akisema “tunaamini kuwa hayatafuta azma ya wasomali ya kuendelea kujenga amani, kujikwamua kiuchumi na kuweka vipaumbele vyao ya usalama.”

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter