Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia wa Cameroon wanaotoroka ghasia kwao bado wanamiminika Nigeria:UNHCR

Familia ya wakimbizi kutoka Cameroon ikiwa nje ya kibanda chao katika makazi ya Adagom, kusini mashariki mwa Nigeria.
UNHCR/Roqan Ojomo
Familia ya wakimbizi kutoka Cameroon ikiwa nje ya kibanda chao katika makazi ya Adagom, kusini mashariki mwa Nigeria.

Raia wa Cameroon wanaotoroka ghasia kwao bado wanamiminika Nigeria:UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Idadi ya wakimbizi wa Cameroon wanaokimbia ghasia nchini mwao na kusaka hifadhi Nigeria sasa imefikia 30,000.

Hayo ni kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi la UNHCR ambalo msemaji wake mjini Geneva, Uswisi, Babar Baloch amewaambia waandishi wa habari kuwa idadi hiyo imeongezeka baada ya wakimbizi takribani 600 kuwasili nchini Nigeria katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Bwana Baloch amesema kuwa wakimbizi hao wanatoroka  maeneo ya Kusini Magharibi na pia Kaskazini Magharibi  yakiwemo Akwaya na Eyumojock ambayo wakazi wake wanazungumza lugha ya kiingereza na waliagizwa kuondoka majumbani mwao kutokana na kukithiri kwa ghasia kwenye maeneo hayo.

 “ Wanne kati ya watano wanaosajiliwa hadi sasa ni wanawake na watoto ambao wamefurushwa kutokana na malalamiko ambayo baadae yaligeuka  ghasia kuanzia mwaka jana.  Wakimbizi hawa wamepewa makazi katika mikoa minne ya Nigeria”

 Machafuko katika maeneo  ya Cameroon yalianza mwaka jana baada ya sauti za kutaka kujitenga kutoka eneo lingine ambalo linazungumza kifanransa na wao huzungumza kiingereza.

UNICEF, ikinukuu makundi yanayotetea haki za binadamu, inasema hadi sasa watu 400 ndio wameuawa  katika makabiliano kati ya makundi yanayotaka kujitenga dhidi ya majeshi ya serikali na UNICEF inaendelea kuwashughulikia wakimbizi  hao kwa kuwapa msaada wa chakula na mahitaji mengine muhimu.

Hata hivyo msimu wa mvua na hali mbaya ya barabara hadi ndani vijijini vinatatiza shughuli zao ambapo watu hao wanahitaji chakula, mahali pa kulala, maji safi na sehemu za usafi.