Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko yanayoendelea Hudaydah ni changamoto kwa raia na watoa misaada:UNHCR/WFP

Raia wa Yemen wakiwa katika mstari wa kusubiri msaada wa kibinadamu uliokuwa ukisambazwa na UNICEF katika maeneo ya Hudaydah mwezi juni 2018.
UNICEF
Raia wa Yemen wakiwa katika mstari wa kusubiri msaada wa kibinadamu uliokuwa ukisambazwa na UNICEF katika maeneo ya Hudaydah mwezi juni 2018.

Machafuko yanayoendelea Hudaydah ni changamoto kwa raia na watoa misaada:UNHCR/WFP

Amani na Usalama

Mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na la mpango wa chakula duniani, WFP leo yameelezea hofu yake dhidi ya kuendelea kwa machafuko kwenye mji wa Hudaydah nchini Yemen na kusema yanaweka njia panda mustakabali wa raia, wakimbizi na operesheni za wahudumu wa misaada ya kibinadamu.

 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis hii leo msemaji wa UNHCR Shabia Mantoo amesema,

“Mapigano makali, mashambulizi ya anga na makombora vimesababisha zahama kubwa kwa raia. Mwezi Oktoba pekee raia 94 wameuawa na 95 kujeruhiwa kwenye jimbo la Hudaydah. Pia kuna uharibifu mkubwa wa miundombinu ya raia ikiwemo vituo vya afya na majumba.”

Shirika hilo linahofia pia machafuko yanayoendelea ni kikwazo kikubwa cha kufikisha mahitaji muhimu ya kibinadamu kwenye jimbo hilo, huku ghala la UNHCR likiwa limejaa msaada ukiwemo vifaa vya malazi .

Nalo shirika la WFP likisisitiza haja ya kumfikia kila anayehitaji msaada wa dharura limesema  la muhimu siyo kusema “tutaongeza msaada mara mbili,” bali tofauti ni tunaweka mipango ili kusaidia watu takribani milioni 14 ili kuepuka janga la njaa kwa mamilioni ya watu. Msemaji wa WFP Geneva ni Herve Verhoosel,

“Hata hivyo hebu tuwe wazi kwamba halitofanyika kwa siku moja. Kwa sasa tayari tunawafikia watu milioni 8 kwa mwezi. Tayari ni mafanikio katika mazingira haya lakini bila shaka matokeo mazuri ni muhimu.”

WFP imetoa wito wa kupatikana fursa za kufika kwenye kituo cha hifadhi ya chakula cha bahari ya Shamu, bandari za Yemen, kusitisha machafuko mara moja na kuhakikisha mishahara ya wafanyakazi wa umma iliyositishwa inalipwa.