UN yaendelea kuhaha kunusuru wakazi wa Hudaidah nchini Yemen

8 Novemba 2018

Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema mapigano yanayoendelea hivi sasa kwenye mji wa Hudaidah nchini Yemen yanazidi kuweka hatarini makumi ya maelfu ya watu na kuzuia shirika hilo kuwafikishia misaada ya dharura wanayohitaji

Mkurugenzi wa WHO  kanda  ya eneo la mashariki mwa Mediteranea Dkt. Ahmed Al-Mandhari amesema hayo leo kupitia taarifa ya shirika hilo iliyotolewa Cairo, Misri.

Amesema mapigano yanayoendelea karibu na maeneo ya hospitali,  yanaathiri misafara ya wahudumu wa afya, wagonjwa na magari ya kusafirisha wagonjwa sambamba na utendaji wa vituo vya afya na hivyo kusababisha mamia ya watu kusalia bila matibabu.

“Ikiwa ni asilimia 50 tu ya vitu vya afya ndio vinafanya kazi nchini Yemen, na hakuna madaktari katika asilimia 18 ya wilaya za Yemen, hatuwezi kukubali hata mhududmu mmoja wa afya auawe au hata hospitali moja ishindwe kutoa huduma,” amesema Dkt. Al-Mandhari.

Amesema mjini Hudaidah,ambao ni mji wa bandari,  hospitali ziko karibu na uwanja wa mapambano na hivyo kuweka hatarini maisha ya wagonjwa na wahudumu wa afya wakati huu.

Nchini Yemen, kwa mujibu wa WHO, tayari nusu ya wakazi wa Yemen hawana uhakika wa chakula na utapiamlo uliokithiri umekumba watoto milioni 1.8 wenye umri wa chini ya miaka mitano na wanawake milioni 1.1 wakiwemo wajawazito na wanaonyonyesha watoto.

Kutokana na mfumo wa afya kudorora Yemen, Dkt. Al-Mandhari amesema tayari wameanzisha vituo vya afya 269 nchini  Yemen pamoja na vituo 51 kwenye majimbo 17 kwa ajili ya lishe il ikuokoa watoto walio na utapiamlo uliokithiri.

Halikadhalika WHO imeweka vituo 72 vya kutibu kipindupinduna vingine 25 vya mgao wa dawa ya kusaidia waliougua kipindupindu kurejesha maji mwilini.

Ametumia fursa hiyo pia kusihi pande kinzani Yemen kuheshimu sheria za kibinadamu kwa mujibu wa sheria za kimataifa akisema sheria hizo zinataka hakikisho la ulinzi wa wahudumu wa afya, vituo vya afya, wagonjwa, magari ya wagonjwa na pia kuwezesha misaada ya kibinadamu kufika haraka kuleta inakohitajika zaidi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter