Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uganda yajihadhari kabla ya shari kwa kuchanja wahudumu wa afya dhidi ya Ebola:WHO

Utoaji chanjo ya Ebola
WHO/S. Hawkey
Utoaji chanjo ya Ebola

Uganda yajihadhari kabla ya shari kwa kuchanja wahudumu wa afya dhidi ya Ebola:WHO

Afya

Kufuatia mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, mara mbili tangu mei mwaka huu, shirika la afya duniani WHO kwa kushirikiana na serikali ya Uganda wameanza kuchukua hatua ya kuwachanja wahudumu wa afya kuepusha kusambaa kwa ugonjwa huo ambapo tayari watu 180 wamethibitishwa kufariki dunia kutokana na Ebola. 

Hatua ya hivi karibuni zaidi ni kutangaza utoaji wa chanjo kwa wahudumu wa afya wapatao 2,100 walio mstari wa mbele katika juhudi za kuzuia virusi vya Ebola kuenea hadi Uganda na kusimamia wagonjwa endapo kisa chochote kitaripotiwa.

Wizara ya Afya ikishirikianna na wadau wengine ikiwemo shirika la Umoja wa Mataifa la Afya, WHO, imetangaza kuwa chanjo hiyo itaanza kutolewa wiki ijayo.

Dkt. Nicholas Kwikiriza Magambo, Kaimu Mkuu wa Afya wa wilaya ya mpakani ya Kikuube ambaye pia ni kiongozi wa kikundi mahsusi cha kufuatilia ebola anafaffanua kuhusu ufuatiliaji wa mlipuko wa Ebola, DRC.

“Mosi tumewafunza wahudumu wa afya kuhusu ufuatiliaji na kuchekecha washukiwa wa ebola, jinsi ya usimamizi wa wagonjwa wa ebola na pia tumetenga kituo maalum cha kushughulikia wagonjwa wa ebola kule Kasonga katika kambi ya Kyangwali. Tumewatuma kwenye mipaka wanakopitia wakimbizi kutoka DRC, ili wachekechwe”

Na kueleza kwa nini juhudi za kinga zimejikita kwenye kambi ya wakimbizi ya Kyangwali.

“Tuko chonjo kwenye makazi ya wakimbizi ya Kyangwali kwa sababu kila siku inapokea wanaokimbia mgogoro DRC hasa katika vijiji mlimoripotiwa mlipuko, mfano Chomya mkoani Ituri”

Kuhusu mchango wa WHO…

“WHO inasaidia serikali kwa kutoa vifaa na msaada wa kitaalamu na kuwezesha shuhuli za ufuatiliaji na kuzuia mlipuko wa ebola”

Timu ya kutoa chanjo dhidi ya Ebola iliyopiga kambi huko kijiji cha Iboko, wakiwa na pipa lenye chanjo wakielekea eneo la Bisolo. Hii ni tarehe 20 juni 2018
WHO/Lindsay Mackenzie
Timu ya kutoa chanjo dhidi ya Ebola iliyopiga kambi huko kijiji cha Iboko, wakiwa na pipa lenye chanjo wakielekea eneo la Bisolo. Hii ni tarehe 20 juni 2018

 

Maeneo ya mpakani yanayofuatiliwa kwa karibu ni pamoja na Buhuka na Sebagoro ambako wakimbizi wanaingilia kupitia kwenye Ziwa Albert.

Mlipuko wa ebola ulimalizia kuripotiwa huku Uganda mwaka 2012 na kusababisha vifo vya watu 14 katika wilaya ya Kibaale.