Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waliopoteza maisha wakijaribu kuvuka Mediterania sasa ni zaidi ya 2000

Waokoaji wa kikosi cha wanamaji cha Italia wakiokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediterania
Italian Coastguard/Massimo Sestini
Waokoaji wa kikosi cha wanamaji cha Italia wakiokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediterania

Waliopoteza maisha wakijaribu kuvuka Mediterania sasa ni zaidi ya 2000

Wahamiaji na Wakimbizi

Idadi ya watu waliopoteza maisha wakivuka baharí ya Mediteranea mwaka huu wakienda kusaka hifadhi Ulaya imevuka 2000  baaada ya maiti 17 kupatikana kwenye ufukwe wa Hispania juma hili.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR imesema hayo katika taarifa iliyotolewa hii leo mjini Geneva Uswisi ikitathmini idadi ya watu waliopoteza maisha mwaka huu pekee na wahamiaji na wakimbizi walioweza kufika barani Ulaya.

Idadi kubwa ya vifo yaani takribani nusu ya vifo vyote vilivyoripotiwa vilitokea katika maeneo ya kuingia nchini Italia ingawa wengi waliofanikiwa kuvuka waliiingia nchini Hispania. Zaidi ya watu 48, 000 wameingia Hispania kwa njia ya bahari, ikilinganishwa na takribani watu 22,000 walioingia Italia na 27,000 walioingia Ugiriki.

UNHCR imekuwa ikitaka hatua za kulitatua suala hili la wahamiaji kupoteza maisha katika harakati za kuzikimbia nchi zao na kutafuta makazi katika nchi za Ulaya kupitia katika njia ya  bahari ya Mediterania ambayo kwa miaka kadhaa imekuwa njia ya hatari zaidi kwa wakimbizi na wahamaji.

Takribani watafuta hifadhi 100,000 na wahamaji wamefika barani Ulaya hadi sasa mwaka huu, ingawa idadi ya vifo ni kubwa ikielezwa kuwa, kwa mwezi Septemba pekee  kwa kila watu 8 waliovuka bahari ya Mediteranea, mmoja alipoteza maisha.

UNHCR inasisitiza kuwa watu wote wanaookolewa katika eneo la maji la kimataifa yaani maili 12 kutoka eneo la maji yaliyoko katika himaya ya Libya, hawatakiwi kurejeshwa nchini Libya ambako hali si shwari.

Shirika hilo pia linarudia tena wito wake kwa jumuiya ya kimataifa kutafuta visababishi vinavyowalazimisha watu kuhama na kupitia njia zile zile za hatari.