Achilieni huru watoto waliotekwa huko Cameroon- UNICEF

6 Novemba 2018

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limetoa wito wa kuachiliwa huru kwa zaidi ya watu 80, wakiwemo watoto wanaoripotiwa kuwa walitekwa kutoka shule moja huko mkoa wa Bamenda ulioko kaskazini-magharibi mwa Cameroon.

Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Afrika Magharibi na Kati, Bi. Marie-Pierre Poirier amesema kupitia taarifa yake kuwa wanalaani vikali shambulio hilo dhidi ya shule na kutaka watoto wote waachiliwe  huru mara moja bila masharti yoyote.

 “UNICEF ina wasiwasi mkubwa kuhusu vitendo hivyo vya ghasia. Mashambulizi dhidi ya shule ni ukiukwaji wa haki za mtoto na pia shule zinapaswa kuwa pahala salama na kupatiwa ulinzi wakati wowote,” amesema Bi. Poirier.

Halikadhalika amezungumzia kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama na kuzidi kupanuka kwa mzozo kwenye mikoa ya Kaskazini-Magharibi na Kusini-Magharibi mwa Cameroon na kutoa wito kwa pande zote husika kuruhusu watoa huduma za kibinadamu waweze kufikisha misaada kwa wakazi walioko kwenye maeneo hayo.

Mzozo umekuwa ukiripotiwa kwenye maeneo hayo ikihusisha mvutano kati ya jamii zinazozungumza kiingereza na zile zinazogungumza kifaransa.

Umoja wa  Mataifa umekuwa ukitaka kusitishwa kwa ghasia hizo.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter