Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Silaha zinazojifyatua zenyewe na kuua binadamu zipigwe marufuku- Guterres

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia jukwaa la wavuti huko Lisbon Ureno leo Jumatatu Novemba 5, 2018
Screenshot
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia jukwaa la wavuti huko Lisbon Ureno leo Jumatatu Novemba 5, 2018

Silaha zinazojifyatua zenyewe na kuua binadamu zipigwe marufuku- Guterres

Amani na Usalama

Maendeleo ya teknolojia za kisasa yana faida na hasara zake kwa maisha ya binadamu hivi sasa kwa hiyo ni lazima kuchukua hatua ili kuhakikisha faida inakuwa kuwa kubwa kuliko hasara.

Amesema hii leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wakati akihutubia jukwaa la wavuti linalofanyika huko Lisbon, Ureno ambapo amesema licha kwamba teknoloja hizo zinarahisisha kazi kama vile utambulisho wa binadamu , kusambaza mgao wa fedha na hata kubaini maeneo yaliyopimwa bado nyingine zinapaswa kuangaliwa upya.

Bwana Guterres ametolea mfano wa akili bandia ambayo inatumika hivi sasa na hata kuwezesha baadhi ya makombora kuweza kuamua eneo ambako linatakiwa kulengwa na hatimaye kufyatuliwa.

Katibu Mkuu amesema “mashine ambazo zina uwezo na utashi wa kuua binadamu hazikubaliki kisiasa, zinachukiza kimaadili na lazima zipigwe marufuku kwa mujibu wa sheria za kimataifa," akisema kuwa kadri akili bandia inavyoingizwa katika masuala ya silaha zinazojiendesha zenyewe na kuchagua eneo la kulenga, itakuwa vigumu kuepukana na kupanua kwa mizozo na kuhakikisha kuwa sheria za kimataifa za kibinadamu na zile za haki za binadamu zinazingatiwa.

Katibu Mkuu amesema hilo ni moja  ya mambo ambayo anaona ni changamoto za kasi ya ukuaji wa teknolojia za hali ya juu.

Teknolojia ya droni nayo inaweza kuwa na manufaa bora au hasara kwa kutegemea inatumika kwenye misingi ipi. Hapa ni kwenye maonyesho ya ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu data uliofanyika Dubai 2018
IISD/ENB
Teknolojia ya droni nayo inaweza kuwa na manufaa bora au hasara kwa kutegemea inatumika kwenye misingi ipi. Hapa ni kwenye maonyesho ya ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu data uliofanyika Dubai 2018

Changamoto nyingine amesema kasi kubwa ya ukuaji wa teknolojia ina athari pande mbili, ambapo kuna watu wanaopoteza ajira na wanaopata ajira na hivyo kuleta ukosefu wa utangamano kwenye jamii akisema, “Tutahitaji uwekezaji mkubwa kwenye elimu, lakini aina mpya ya elimu. Jambo muhimu sasa si kujifunza mambo bali kujifunza namna ya kujifunza mambo. Tutatambua kuwa watu wengi watapata stadi za kuwawezesha kupata taaluma mpya, lakini baadhi watabaki nyuma. Tutalazimisha aina mpya ya mbinu za hifadhi ya jamii ili waweze kuishi na kuona umuhimu wa maisha yao."

Katibu Mkuu amesema hilo ni eneo linalotia hofu kubwa na hivyo ni vyema kuhamasisha serikali, mashirika ya kiraia na kila mtu lakini hatua hazichukuliwe kwa kasi inayotakiwa ili kutekeleza jambo hilo.

Suala lingine ambalo Katibu Mkuu ameona ni changamoto kile kinachotajwa kuwa ni matumizi  yasiyo sahihi ya mitandao ikiwemo faragha za watu kuingiliwa, kauli za chuki na kibaguzi kuenezwa sambamba na ulaghai katika masuala ya uchaguzi.

Hata hivyo amesema, hivi vina mizizi yake, na huwezi kulaumu wavuti kwa hali hii. Lakini ni kweli kwamba wavuti unatumika tu kupanua tatizo hili, na tunahitaji kuhamasisha serikali, mashirika ya  kiraia, wasomi na wanasayansi ili tuweze kuzuia matumizi ya kilaghai ya kidijitali kwenye uchaguzi kwa mfano na kuweka vidhibiti vitakavyozuia kauli za chuki kuwa chanzo cha ukosefu wa utulivu kwenye jamii.”

Mkutano huo wa siku nne umeleta pamoja wabobezi wa teknolojia, na wafanyabiashara.