Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Saudia yajutia mauaji ya Khashoggi

Dkt.Bandar bin Mohammed Al-Aiban, rais wa Kamishna ya Haki za Binadamu, Saudia na mkuu wa ujumbe wa Saudia kwenye kikao cha 31 cha kutathmini haki uliofanyika Geneva Uswis, Novemba 5, 2018
UN Geneva/Daniel Johnson
Dkt.Bandar bin Mohammed Al-Aiban, rais wa Kamishna ya Haki za Binadamu, Saudia na mkuu wa ujumbe wa Saudia kwenye kikao cha 31 cha kutathmini haki uliofanyika Geneva Uswis, Novemba 5, 2018

Saudia yajutia mauaji ya Khashoggi

Haki za binadamu

Saudi Arabia imeelezea “kujuta na machungu” kwa mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi, wakati wa mkutano wa tathimini uliofanyika leo mjini Geneva Uswis na huku ikisisitiza ahadi yake ya kufikia "viwango vya juu zaidi" katika masuala ya haki za binadamu nchini humo, ikiwa ni pamoja na haki za wanawake na wahamiaji.

Akithibitisha kwamba uchunguzi bado unaendelea kufuatia mauaji ya Khashoggi ambaye mara ya mwisho alionekana akiingia kwenye ubalozi mdogo wa Saudia mjini Instanbul, Uturuki tarehe 2 Oktoba, Dkt. Bandar bin Mohammed Al-Aiban amewaambia nchi wanachama kwamba Mfalme Abdel-Aziz ndiye aliyeanzisha uchunguzi huo. Na kuongeza kuwa “Saudi Arabia tayari imeshaelezea majuto na machungu yake kuhusu mauaji ya Jamal Khashoggi, na Mfalme Abdel-Aziz ameshawaamuru uwajibikaji na uchunguzi wa kesi hii kwa mujibu wa sheria stahiki na maandalizi ya kupata ukweli wote na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wahusika ili kuweka bayana ukweli wote kwa umma.”

Kufuatia maelezo hayo ya Dkt. Al-Aiban, nchi 40 wanachama waiomba, kubaini ukweli wa nini kilichotokea kwa Bwana Khashoggi, huku wengine wengi wakiomba kufanyiwa marekebisho ya sheria za uhuru wa kujieleza katika Ufalme huo.

Takriban nchi 10 pia zimeelezea hofu yake kuhusu mgogoro wa kibinadamu unaoendelea nchini Yemen ambako Saudi Arabia imekosolewa kwa kuratibu mashambulizi ya anga yaliyokatili maisha ya raia wengi.

Kuhusu suala hilo la Yemen Dkt. Al-Aiban amesisitiza kuwa Saudi Arabia “Inaendelea na msimamo wake wa kuwasaidia watu wa Yemen na serikali yao halali “ ambaye amesema iliomba usaidizi dhidi ya wapiganaji wa Houthi mwaka 2015.

Ameongeza kuwa “Vikosi vya muungano vinafanya kila liwezekanalo kuwalinda raia hususan wanawake na watoto , maeneo ya raia, na miundombinu kutokana na athari za vita. Amesema familia za Saudi zilizoko kwenye mpaka na Yemen zimeendelea kuathirika na mashambulizi ya wapiganaji wa Houthi  na kusisitiza haja na dhamira ya nchi kushirikiana na jumuiya ya kimataifa kufikisha msaada unaohitajika kwa watu wa Yemen zaidi ya milioni 14 wanakabiliwa na njanga la njaa kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Dkt. Al- Aiban amesema Ufalme wa Saudia umekuwa ukitoa msaada ambao umefikia dola bilioni 11 tangu mwaka 2015.

Jumla ya nchi 97 zimezungumza katika tathimini hiyo ya Umoja wa Mataifa (UPR) kuhusu Saudi Arabia mjini Geneva.

Dkt. Al-Aiban amesema Saudi Arabia imekubali mapendekezo Zaidi ya 150 yaliyowasilishwa katika tathimini iliyopita , na pia imekubali shememu ya mapendekezo mengine 37.

Kwa mujibu wa wa sharia za UPR nchi zote 193 wanachama zinafanyiwa tathmini na wenzao na kila mwaka nchi 42 zinatathminiwa.

Chombo hicho hukutana mara tatu kwa mwaka na kutoa taarifa kwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Kwa nchi ambazo zimetathiminiwa pia hupokea mapendekezo ambayo zinatarajiwa kuyatekeleza kabla ya tathimini ya mwaka unaofuata.