Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP na Alibaba waingia ubia kufanikisha lengo namba mbili la SDGs la kutokomeza njaa.

Mgao wa chakula wa WFP kwa wahusika.
WFP/Photolibrary
Mgao wa chakula wa WFP kwa wahusika.

WFP na Alibaba waingia ubia kufanikisha lengo namba mbili la SDGs la kutokomeza njaa.

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la mpango wa chakula duniani WFP limeingia ushirika  na kampuni ya Alibaba, inayoongoza duniani kwa biashara mtandao au E-Commerce, ushirika ambao utasaidia juhudi za kufanikisha lengo namba mbili la maendeleo endelevu SDG la kutokomeza njaa ifikapo mwaka 2030.

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo mjini Hangzhou China,yaliko makao makuu ya Alibaba, imesema  kuwa mkataba wa ushirikiano umetiwa sahihi na David Beasley, Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, na Mwenyekiti wa Alibaba Sun Lijun.

Chini ya mkataba huo, Alibaba itatoa teknolojia yake ya kisasa kusaidia  kazi za WFP  ambapo  kupitia tawi lake la  teknolojia la Alibaba-Alibaba Cloud, itashirikiana na WFP kuunda ramani ya kidijitali inayoonyesha maeneo yenye njaa ili kuweza kujua hali ya njaa duniani na pia kusaidia kuboresha kazi kwa kusaidia juhudi kuelekea kufanikisha kutokomeza njaa duniani ifikapo mwaka wa 2030.

 Akizungumza katika hafla hiyo, Bwana Lijun amesema kutokomeza umaskini duniani pamoja na kukabiliana na njaa  ni lengo ambalo Alibaba linachangia na WFP, “tuko tayari kuungana katika kampeni ya dunia ya vita dhidi ya njaa kwa kutumia teknolojia yetu bunifu kuhusu data pamoja na kubadilishana uzoefu sio tu nchini China bali na duniani kote.”

Kwa upande wake mkuu wa WFP, Bwana Beasley, amaeupongeza ubia huo na kusema ni hatua moja mbele  katika kuimarisha uhusiano kati ya WFP na sekta binafsi ya China.

“ Sasa tuna mshirika mkuu katika vita dhidi ya njaa, mchango na uzoefu wa kampuni tanzu ya Alibaba kama vile uwezo wa kuchanganua takwimu na jukwaa la mtandaoni vitasadia sana WFP katika juhudi zake za kupunguza njaa duniani ambayo imekuwa ikizidi kupanda.”

Lengo la “ramani ya kidijitali ya njaa duniani” ni kuchunguza data ili kusaidia WFP kuboresha makadirio yao na kuongeza uchunguzi wake na kupunguza muda wa kuingilia kati wakati wa dharura. Kazi itaratibiwa pamoja na pande zote kwa kuweka kundi la pamoja  la “dijitali ya kuleta mabadiliko” kuweza  kuchunguza nafasi mpya.