FAO kuwasaidia waathirika wa Tsunami Indonesia

5 Novemba 2018

Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO limezindua mpango utakaowasaidia  zaidi ya wakulima 70,000 wa Indonesia  pamoja na wafuga wa samaki kuweza kurudia kazi zao za zamani baada ya tetemeko la ardhi na tsunami vilivyosambaratisha mbinu za kukwamua maisha yao.

Taarifa iliyotolewa leo na FAO huko Roma Italia, Jakarta- Indonesia pamoja na Bangkok Thailand, inasema uzinduzi huo umechochewa na  madhara makubwa ya tetemeko la ardhi la mwezi Septemba mwaka huu, tetemeko ambalo ni  baya kuwahi kutokea nchini humo kwa kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.

Watu zaidi ya 200,000 walipoteza makazi yao na wengine 3,000 walifariki dunia au hawajulikani waliko kutokana na tetemeko hilo la ardhi na tsunami.

Katika kipindi cha miezi mitatu ijayo, FAO inapanga kuwafikia wakulima 50,000 na kuwapatia mbegu za mchicha na mbolea na vitendea kazi kama vile majembe na koleo ili kuanza kulima kwa minajili ya kujitosheleza kwa chakula.  Halikadhalika wavuvi takriban 20,000 watapewa vifaa  vya kuwasaidia kuvua samaki.

FAO inasema familia ambazo zitanufaika na mpango huo ni zile ambazo ziko katika maeneo yaliyoathirika sana na majanga hayo ya Donggala, Sigi, Paluna Parigi Moutong katika mkoa wa Sulawesi kati.

Shirika hilo pia linapanga kutoa msaada wa pesa taslim kwa wanawake 4,000 ambao ni wajawazito na vilevile wanawake na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ili kuwawezesha kupata chakula chenye lishe.

Mwakilishi wa FAO nchini Indonesia,Stephen Rudgard, amesema kuwa familia nyingi katika mkoa wa Saluwesi ya Kati hutegemea mno kilimo na uvuvi na kwa wengi hii ndiyo tegemeo lao pekee la chakula na pato, na sasa hayo yote sasa yametokomea.

 Akaongeza, “ tunajua kuwa watu wengi nchini Indonesia wamepitia hali ngumu na ni watu wavumilivu lakini ni  muhimu kwa FAO kujitokeza kusaidia juhudi za serikali za kuwasaidia watu wa Saluwesi kuweza kujikwamua kutoka hali waliyomo."

Hadi sasa inakisiwa kuwa  hekta 10,000 za ardhi inayotumiwa kwa kilimo ziliharibiwa ambapo mashamba ya  mpunga na mahindi ndiyo yaliathirika vibaya. Uharibifu  wa mfumo wa unyunyuziaji wa maji katika wilaya ya Sigi ulikata maji kwa ardhi ya kulimwa ya ukubwa wa hekta 8,000.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter