Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kufa kwao kunatukumbusha jukumu letu la kuendelea kuwalinda wananchi wa Mali : Gyllensporre

Msafara wa walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakiwa kazini.
MINUSMA/Harandane Dicko
Msafara wa walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakiwa kazini.

Kufa kwao kunatukumbusha jukumu letu la kuendelea kuwalinda wananchi wa Mali : Gyllensporre

Amani na Usalama

Askari wawili wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuleta amani nchini Mali, MINUSMA waliouawa katika shambulizi la kushitukiza juma lililopita, wameagwa na wenzao hii leo mjini Bamako nchini humo.

Walinda amani wawili kutoka Burkina Faso waliuawa mwezi uliopita Oktoba 27 wakiwa katika kambi ya MINUSMA huko Ber, eneo la Timbuktu nchini Mali. Walinda amani wengine pia wa Burkina Faso walijeruhiwa katika shambulizi hilo. Siku hiyo hiyo pia walinda amani kutoka Togo walijeruhiwa katika shambulizi jingine dhidi ya MINUSMA kwenye eneo la Konna huko Mopti nchini humo Mali.

Katika hafla hiyo ameagwa pia mlinda amani kutoka Guinea ambaye alifariki dunia kutoka na kuugua akiwa kazini huko Kidal.

Kabla ya kusafirishwa kwa ndege mpaka Burkina Faso na Guinea, majeneza matatu yaliyozungushiwa bendera za Umoja wa Mataifa yameoneshwa katika kambi ya MINUSMA iliyoko katika mji mkuu wa Mali, Bamako.

Kamanda mkuu wa MINUSMA, Luteni Jenerali Dennis Gyllensporre ameongoza shughuli hiyo ya kuwaaga askari wake akiwa na wawakilishi kutoka jeshi la Mali.

Gillensporre ametoa heshima zake kwa askari hao watatu waliojitolea maisha yao ili kutunza amani kupitia Umoja wa Mataifa na akiwahutubia waombolezaji amesema, “Leo ni siku ya huzuni mkubwa. Lakini kama kamanda wa MINUSMA, ninawashukuru askari hawa kwa nguvu yao ambayo inatukumbusha kuhusu jukumu letu la kuwalinda watu wa Mali”

Aidha Luteni Jenerali Gyllensporre ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza watu wao na akawatakia ahuweni ya haraka askari wengine walionusurika katika mashambulizi hayo, pia akiwaapongeza kwa ushujaa wao.

Kundi la maafisa polisi wa UN waliopo ujumbe wa UN wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA, wakizungumza na raia wakati wa doria mjini Menaka, kaskazini mwa Mali.
UN /Marco Dormino
Kundi la maafisa polisi wa UN waliopo ujumbe wa UN wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA, wakizungumza na raia wakati wa doria mjini Menaka, kaskazini mwa Mali.

 

Tukio hilo liliambatana na ukimya wa dakika moja ili kuwaenzi askari hao kisha kamanda mkuu akaweka shada la maua katika kila jeneza na kuwatunuku medali za Umoja wa Mataifa askari hao waliolala.

MINUSMA ilianzishwa ili kutuliza ghasia na kuleta amani na utulivu nchini Mali kutokana na jaribio la mapinduzi la mwaka 2012 ambapo eneo la kaskazini mwa nchi lilitwaliwa na waasi.