Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania ilinde wapenzi wa jinsia moja badala ya kuwaweka hatarini- Bachelet

Bendera ya LGBT. Picha: UM

Tanzania ilinde wapenzi wa jinsia moja badala ya kuwaweka hatarini- Bachelet

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet ameeleza wasiwasi wake kufuatia taarifa ya kwamba mkuu wa mkoa wa Dar es salaam nchini Tanzania ataunda kamati ya kufuatilia na kukamata mashoga na wale wanaoshukiwa kuwa na mwenendo huo.

Taarifa ya ofisi ya haki za binadamu iliyotolewa leo mjini Geneva, USwisi  imemnukuu Bi. Bachelet akisema kuwa “wasagaji, mashoga, wenye uhusiano wa pande mbili na waliobadili jinsia zao nchini  Tanzania tayari wamekuwa wakikabiliwa na ghasia, unyanyasaji na ubaguzi kwa miaka miwili sasa.”

Na kama hiyo haitoshi amesema, “wale ambao wanatetea haki za kiafya, za kuishi bila kubaguliwa, kutokukabilia na ghasia na hata kukamatwa kiholela nao pia wamekuwa wakilengwa na kukamatwa.”

Kamishna Mkuu amesema kitendo hicho dhidi ya kundi la LGBT kinaweza kugeuka na kuwa leseni ya kuwafanyia ghasia, kuwatisha,kuwanyanyasa na kuwabagua watu hao.

Bi. Bachelet amesihi serikali ya Tanzania itekeleze wajibu wake wa kulinda haki za watu wote ndani ya nchi hiyo ikiwemo kuwajibisha wale wanaopigia chepuo chuki na ubaguzi pamoja na wale wanaofanya ghasia dhidi yaw engine.

“Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari, watoa huduma za afya wanaweza kutekeleza kazi zao adhimu bila kushambuliwa au kuteswa.

 

Image
Sao Mimol ampiga busu mwenzie mbele ya Bendera ya LGBT wakati wa mkutano huko Tekeo. Alikuwa na umri wa Miaka 20 alipogundua kwamba anavutiwa na wanawake wenzake na ilikuwa vigumu wakati huo kujitokezea na na kupata haki za za LGBT. Picha: UN Women/Mariken Harbitz

Mpango uliotangazwa na serikali ya Tanzania unajumuisha kuwabadilisha au kuwatibu mashonga, kitendo ambacho kinaelezwa kuwa ni hatarishi na kinyume na maadili, kwa mujibu wa Kamati dhidi ya utesaji na shirika la afya ulimwenguni, WHO.

Bi. Bachelet amesema kitendo hicho nacho kinaweza kunyanyapaa zaidi mashoga.

“Natoa wito kwa serikali  na wananchi wa Tanzania kusimama kidete kutetea haki za binadamu za kila mtu nchini humo, bila kujali ni nani wanayempenda,” amesema Bi. Bachelet akiongeza kuwa “viongozi wa kisiasa, kidini na wengineo wanapaswa kufanya kazi kuondokana na fikra hizi potofu kwa misingi ya jinsia na utambulizi wa mtu.”

Halikadhalika Kamishna Mkuu ametoa wito wa kuangaliwa upya kwa sheria zinazoharamisha mahusiano kati ya watu wa jinsia moja.