Mwaka 2018 pekee waandishi 88 wameuawa hadi sasa

Kampeni ya UNESCO ikisema "Ukweli katu haufi" ikiwa ni kampeni ya kutokomeza ukwepaji sheria kwa vitendo vya mauaji dhidi ya waandishi wa habari
UNESCO
Kampeni ya UNESCO ikisema "Ukweli katu haufi" ikiwa ni kampeni ya kutokomeza ukwepaji sheria kwa vitendo vya mauaji dhidi ya waandishi wa habari

Mwaka 2018 pekee waandishi 88 wameuawa hadi sasa

Haki za binadamu

Katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja waandishi habari takriban elfu moja  wameuawa wakati wanafanya kazi yao adhimu, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya kukomesha ukwepaji sheria kwa uhalifu dhidi ya waandishi wa habari.

Bwana Guterres anasema jambo baya zaidi ni kwamba hadi sasa kesi tisa kati ya kumi hazijatatuliwa  na hakuna mtu yeyote  ambaye amewajibishwa.

Katibu Mkuu anasema, “waandishi wa habari wa kike mara nyingi wako katika hatari  zaidi ya  kulengwa si tu kwa sababu ya kuandika habari bali pia kwa sababu ya jinsia yao, ikiwemo kupitia vitisho vya ukatili wa kingono.”

Amesema vitisho pia vinaambatana na mauaij ambapo mwaka huu pekee takribani waandishi wa habari 88 wameuawa na “maelfu kadhaa wameshambuliwa, wamenyanyaswa, wameshikiliwa, ama wamefungwa jela kwa makosa ya ajabu ajabu bila ya mchakato sahihi.”

“Hali hii ni inatisha. Haipaswi kugeuzwa kuwa  kama  hali ya kawaida. Endapo waandishi wa habari wanalengwa, jamii huathirika,” anasema Bwana Guterres akiongeza kuwa , “nasikitishwa na ongezeko la visa vya mashambulio na utamaduni wa kutojali na ukwepaji sheria.”

Image
Komesha ukatili dhidi ya waandishi wa habari. Picha: UNESCO

Katibu Mkuu ametoa wito kwa serikali pamoja na jamii ya kimataifa kuwalinda wandishi habari na pia kuweka mazingira bora wanayohitaji kwa ajili ya kufanya kazi zao.

Ametumia pia ujumbe wake wa leo kuwapongeza waandishi wa habari ambao wanafanya kazi zao kila siku licha ya kudhalilishwa pamoja na vitisho.

“Kazi zao pamoja na za wenzao waliofariki dunia hutukumbusha kuwa katu ukweli haufi. Vivyo  hivyo azma yetu kuhusu haki ya msingi ya uhuru wa kujieleza.  Kuandika habari si kosa, amesema Bwana Guterres akisihi kwamba katika siku  ya leo, “hebu na tusimame kidete na waandishi wa habari kwa ajili ya ukweli na haki.”