Skip to main content

Guterres aongoza kumbukizi ya waliouawa Pittsburg

Watoto wakiwa wamevalia tisheti zenye ujumbe wa kuungana dhidi ya chuki, wakati wa kuwakumbuka waliouawa katika sinagogi.
UN Photo/Rick Bajornas)
Watoto wakiwa wamevalia tisheti zenye ujumbe wa kuungana dhidi ya chuki, wakati wa kuwakumbuka waliouawa katika sinagogi.

Guterres aongoza kumbukizi ya waliouawa Pittsburg

Amani na Usalama

Jijini New York Marekani hii leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameungana na viongozi wengine wa dini na wakazi wa jiji hilo kukumbuka watu 11 waliopoteza maisha katika shambulio la mwishoni mwa wiki kwenye sinagogi moja huko Pittsburg, jimboni Pennyslvania nchini Marekani.

Shambulizi hilo la risasi lililotekelezwa na mtu mmoja aliyekuwa na bunduki katika sinagogi lifahamikalo kama Tree of Life yaani Mti wa Uhai mjini Pittsburgh Pennysylivania Marekani siku ya sabato, pamoja na kusababisha vifo vya watu 11, watu wengine sita walijeruhiwa.

Tukio hili la kuwakumbuka waliopoteza maisha lililopewa jina “Muungano dhidi ya chuki, limefunguliwa kwa wimbo Ose Shalom ambao una maana ya ‘tengeneza amani’ ukiimbwa kwa kiebrania na kwaya ya watoto wa shule ya Park East.

Zaidi ya watu 200 wamekusanyika kwenye sinagogi la kihistoria eneo la Mahattan jijini New York wakiwemo viongozi mbalimbali wa imani tofauti tofauti na madhehebu ambao wameungana na wanadiplomasia na watu wengine ili kuhamasisha jamii zote kuungana pamoja dhidi ya chuki.

Akihamasisha umoja dhidi ya ubaguzi unaoelekezwa kwa wayahudi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema, “tangu niliposhika nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nimekuwa nikipaza sauti dhidi ya kile ninachoamini ni kukua kwa ubaguzi dhi ya wayahudi katika nyingi ya jamii zetu na hasa katika eneo langu la Ulaya lakini pia zaidi katika Amerika kaskazini.”

Akirejelea aina nyingine za chuki dhidi ya dini ikiwemo dhidi ya uislamu na ukristo duniani kote, Guterres amesema chuki dhidi ya imani ya kiyahudi ni ya zamani zaidi na ni imedumu kwa muda katika historia ya mwanadamu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres  akihutubia kongamano lililowakutanisha viongozi mbalimbali wa kiimani kuwakumbuka waliouawa katika sinagogi
UN Photo/Rick Bajornas)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia kongamano lililowakutanisha viongozi mbalimbali wa kiimani kuwakumbuka waliouawa katika sinagogi

Kiongozi mkuu wa sinagogi ambako tukio la leo limefanyika, Rabbi Arthur Schneier ambaye pia ni manusura wa mauaji dhidi ya wayahudi nchini ujerumani pia ambaye familia yake iliuawa katika kambi za Nazi nchini ujerumani katika zama za Hitler amesema, “Nimepitia mabaya. Nimeona mazuri ya mwanadamu na mabaya yake, na mazuri  ya mwanaadamu yatashinda”

Naye Sheikh Musa Drammeh mwenyekiti wa kituo cha utamaduni wa kiislamu cha Amerika Kaskazini amesema, “Ni wakati wa taifa hili kusimama na kuufanya muungano huu, muungano ulio thabiti zaidi na kuzuia chuki.”

Viongozi wa kidini kutoka madhehebu mbalimbali wakiwa pamoja katika sinagogi la Park East mjini New York Marekani kuwakumbuka waliouawa katika sinagogi la wayahudi huko Pennsylvania.
UN Photo/Rick Bajornas)
Viongozi wa kidini kutoka madhehebu mbalimbali wakiwa pamoja katika sinagogi la Park East mjini New York Marekani kuwakumbuka waliouawa katika sinagogi la wayahudi huko Pennsylvania.

 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye aliwahi kuwa Kamishna Mkuu wa Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa,  UNHCR amesema amefanya kazi kwa ukaribu na shirika linatoa msaada kwa wakimbizi wa kiyahudi Hebrew Immigrant Aid Society (HIAS) na limefanya kazi nzuri aliyoiheshimu na kutokana na msaada ambao sinanogi lililoshambuliwa lililokuwa linautoa kwa shirika hilo, ni moja ya sababu ambazo zilimfanya mshambuliaji kushambulia sinagogi hilo.

Viongozi wengine wa kidini waliohudhuria, wameeleza kukataa kwao kila aina ya vurugu, kukosa kuvumiliana na ubaguzi dhidi ya Imani ya kiyahudi, akiwemo Kaldinali Timothy Dolan, Askofu Mkuu wa New York Demestrios, mkuu wa Kanisa la Orthodox tawi la America na Askofu Auza, mwakilishi wa kudumu wa Papa katika Umoja wa Mataifa.