Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Twataka pande kinzani Yemen zikutane ndani ya mwezi mmoja- Griffiths

Vijana wa kiume wakiwa wamesimama katika jengo lililobomolewa sehemu za Saada Yemen.
WFP/Jonathan Dumont
Vijana wa kiume wakiwa wamesimama katika jengo lililobomolewa sehemu za Saada Yemen.

Twataka pande kinzani Yemen zikutane ndani ya mwezi mmoja- Griffiths

Amani na Usalama

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Yemen Martin Griffiths amekaribisha wito wa hivi  karibuni wa kutaka kuanza tena kwa mchakato wa kisiasa nchini Yemen pamoja na hatua za kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano nchini humo.

Taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya Bwana Griffiths imemnukuu akisisitiza kuwa “ hakuwezi kuwepo na suluhu la kijeshi kwenye mzozo wa Yemen. Nitaendelea kufanya kazi na pande zote kukubaliana juu ya hatua bora za kuepusha wayemen dhidi ya madhara ya mzozo unaoendelea kukumba nchi yao.”

Ametaka pande zote zishughulikie kwa udharura janga la kisiasa, kiusalama na kibinadamu nchini Yemen wakati huu ambapo  inaelezwa kuwa takribani nusu ya wakazi wa nchi hiyo hawana uhakika wa wapi watapa chakula.

“Nasihi pande kinzani zitumie fursa ya sasa kujihusisha ipasavyo na juhudi zetu za sasa na kurejesha haraka mashauriano ya kisiasa ili kukubaliana juu ya muundo wa mashauriano hayo, hatua za kujengeana imani hususan kuimarisha uwezo wa Benki Kuu ya Yemen, kubadilishana wafungwa na kufungua tena kwa uwanja wa ndege wa Sana’a,” amesema mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa.

“Natiwa moyo na ushiriki chanya wa serikali ya Yemen na Ansarullah na nitaendelea kushirikiana na pande zote husika kwenye ukanda huu ili hatimaye kuwepo na suluhu jumuishi ya kisiasa ya kumaliza mzozo wa Yemen,” amesema Bwana Griffiths.

Amehitimisha kwa kusema kuwa bado wamesalia na azma ya kuleta pamoja pande kinzani za Yemen ndani ya mwezi mmoja ujao akisema mazungumzo ndio njia pekee ya kufikia makubaliano jumuishi.