Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nyaraka za kulinda miji tunazo, tuchukue hatua- Guterres

Mafuriko katika viunga vya mji mkuu wa Thailand, Bangkok miaka kadhaa iliyopita. Hivi sasa mji huo umebuni namna ya kukusanya maji chini ya ardhi na kuyatumia wakati wa ukame.
ESCAP Photo
Mafuriko katika viunga vya mji mkuu wa Thailand, Bangkok miaka kadhaa iliyopita. Hivi sasa mji huo umebuni namna ya kukusanya maji chini ya ardhi na kuyatumia wakati wa ukame.

Nyaraka za kulinda miji tunazo, tuchukue hatua- Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Leo ni siku ya miji duniani ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake alioutoa kuiadhimisha siku hii, ametoa wito kwa dunia nzima kufanya kazi pamoja kujenga miji endelevu na stahimilivu ambayo inawapatia watu wote usalama na fursa. Taarifa zaidi na John  Kibego

Ajenda ya mwaka 2030 kwa ajili ya maendeleo endelevu, mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, mfumo wa Sendai kwa ajili ya kupunguza hatari ya maafa, na ajenda mpya ya miji, kwa pamoja amesema Katibu Mkuu Guterres, vinaleta ramani kwa ajili ya dunia endelevu na stahimilivu.

Katibu Mkuu pia amefafanua kuwa uzingatiaji wa nyaraka hizo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa kila wiki watu milioni 1.4 kote duniani wanahamia mijini  hivyo ukuaji huo wa haraka wa miji unaweza kukwamisha uwezo wa ndani na pia kusababisha ongezeko la hatari zaidi ya majanga ya asili na yale yanayosababishwa na wanadamu.

Hata hivyo amepongeza baadhi ya majiji ambayo  yameshaanza kuchukua hatua akitaja jiji la Bangkok nchini Thailand ambalo limejenga mfumo wa kukusanya maji chini ya ardhi ili kupambana na hatari ya mafuriko na maji hayo yanatumika wakati wa ukame.

Pia ameutaja Quito, mji mkuu wa Equador ambako wameamua kutunza zaidi ya eka laki mbili za ardhi ili kuzuia mafuriko, kupunguza mmomonyoko na kulinda maji safi ya mji na viumbehai.

Wakati Katibu Mkuu akisisitiza umuhimu huo wa kuchukua hatua ili kuwa na majiji endelevu na stahimilivu mtoto Emerson Chong wa Malaysia mwenye umri wa miaka 10 anatambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kwa juhudi zake za kulinda mazingira akitumia sanaa ya uchoraji vikaragosi.

Moja ya kazi yake iliyopewa jina “Earth Boy” ilichapishwa na UNICEF kama sehemu ya kampeni za kuwafundisha watoto kuhusu maendeleo endelevu ambapo Emerson anasema,

“Sina mamlaka yoyote lakini ninaweza kuwavutia au kuwapa msukumo wengine”