Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya wahamiaji 97,000 wavuka Mediteranea mwaka huu pekee kusaka maisha bora Ulaya

Picha ya maktaba katika bahari ya Mediterania, boti ikiwa imewabeba wahamaji na wanaotafuta hifadhi.
UNHCR/L.Boldrini
Picha ya maktaba katika bahari ya Mediterania, boti ikiwa imewabeba wahamaji na wanaotafuta hifadhi.

Zaidi ya wahamiaji 97,000 wavuka Mediteranea mwaka huu pekee kusaka maisha bora Ulaya

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM,  limesema idadi ya wahamiaji na wakimbizi walioingia Ulaya kwa njia ya bahari kuanzia Januari mosi hadi tarehe 28 mwezi huu wa Oktoba ni 97,857 ikionyesha kuwa imepungua ikilinganishwa na 147,170 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Taarifa ya IOM iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi hii leo inasema idadi kubwa ya walioingia Ulaya mwaka huu walipitia Hispania ambapo ilikuwa wakimbizi na wahamiaji 47,433, ikiwa ni sawa na asilimia 48 ya idadi ya wote walioingia Ulaya.

Aidha taarifa hiyo imeweka wazi kuwa njia ya kuelekea Ulaya kupitia bahari ya Mediteranea inasalia kuwa njia ya hatari kwa wahamaji ingawa kwamba idadi ya wanaoutumia njia hiyo imepungua.

Mradi wa IOM unaohusu wahamaji waliopotea umehifadhi kumbukumbu hadi tarehe 28 mwezi huu wa Oktoba ukionyesha vifo 1,987 vya wahamaji, zaidi ya theluthi mbili ya vifo vilivyotokea kati ya Afrika kaskazini na Sicily nchini Italia.

Ingawa hivyo, idadi ya vifo ikilinganishwa mwaka huu na miaka iliyotangulia ni ndogo ambapo mwaka 2017 ilikuwa vifo 2,844 na kwa mwaka 2016 vilitokea vifo 4,039.

Soundcloud