Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utajiri wa taifa siyo kigezo cha elimu bora-UNICEF

Watoto wakijisomea darasani
World Bank/Irina Oleinik
Watoto wakijisomea darasani

Utajiri wa taifa siyo kigezo cha elimu bora-UNICEF

Utamaduni na Elimu

Kuishi katika nchi tajiri siyo kigezo cha usawa wa upatikanaji wa elimu bora, hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya UNICEF iliyotolewa leo mjini Florence Italia na New York Marekani, ikiwa imeangazia ukosefu wa usawa katika elimu kwenye nchi tajiri.

Ikipatiwa jina mwanzo  usio sawa;ukosefu wa usawa wa elimu kwa watoto walio kwenye nchi tajiri, ripoti inazipanga kwenye orodha nchi 41 za Muungano wa Ulaya na shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo, OECD kwa vigezo vya elimu ya awali, msingi na sekondari.

Vigezo hivyo vilitumika kuchunguza uhusiano kati ya mafanikio ya mtoto na masuala kama vile kiwango cha elimu na ajira ya wazazi, historia ya uhamaji, jinsi na mwenendo wa shule.

Katika nchi 16 kati ya 19 za Ulaya ambazo takwimu zake zipo, watoto kutoka katika familia maskini wana idadi ndogo ya kujiunga na shule ya awali kuliko watoto kutoka familia zenye kipato.

Ripoti inasema kuwa kati ya watoto wenye umri wa miaka 15 ambao wanafanya vizuri shuleni, wale wenye wazazi wanaofanya kazi nzuri wana nafasi kubwa ya kuendelea na elimu ya juu kuliko wale wazazi wenye kazi za chini.

Ripoti imeeleza kuwa watoto katika nchi zenye utajiri mdogo mara nyingi wanafanya vema katika masomo yao pamoja na uhaba wa rasilimali ikilinganishwa na wenzao katika nchi tajiri.

“Kile kinachooneshwa na ripoti yetu ni kuwa nchi zinaweza kuwapatia watoto wake ubora wa pande zote , yaani wanaweza kuvifikia viwango vya ubora katika elimu na wakawa na kiwango kidogo cha ukosefu wa usawa, lakini nchi zote tajiri zinaweza na zinatakiwa kufanya zaidi kwa ajili ya watoto wanaotoka katika familia zenye hali mbaya kwani hao ndiyo wako katika uwezekano wa kushindwa” amesema Dkt. Priscilla Idele mkurugenzi wa kitengo cha UNICEF kinachohusika na utafiti huo uliopatiwa jina Innocenti.

Wasichana katika nchi zote wanafanya vizuri zaidi katika majaribio ya kusoma kuliko wavulana. Pengo hili huzidi kuwa kwa kadri watoto wanavyozidi kuongezeka umri lakini kuna tofauti kati ya nchi na nchi, ripoti imesema.

Ili kurekebisha hali ya sasa, ripoti inapendekeza kuhakikisha elimu ya ubora wa juu kwa elimu ya awali na kuwajali watoto, kupunguza pengo la walionacho na wasionacho, kuondoa pengo katika mafanikio ya wasichana na wavulana na kuzingatia usawa na siyo tu na siyo kujali viwango vya wastani.