Chonde chonde Saudia sitisheni hukumu ya kifo kwa watoto:UN

29 Oktoba 2018

Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameitaka serikali ya Saudi Arabia kusitisha mara moja utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa watu sita waliohukumiwa kufa kwa madai ya kufanya uhalifu walipokuwa na umri wa chini ya miaka 18.

Bwana. Ali al-Nimr, Dawood al-Marhoon, Abdullah al-Zaher, Mujtaba al-Sweikat, Salman Qureish na Abdulkarim al-Hawaj wanakabiliwa na kunyongwa wakati wowote.

Watu hao walikamatwa na kuhukumiwa kifo kwa madai mbayo wataalam hao waliyachukulia hapo awali kama yanawasilisha uharamishaji wa kutekeleza haki za msingi ikiwa ni pamoja na haki ya uhuru wa kukusanyika na kujieleza  kwa watu hao waliokuwa na umri wa chini ya miaka 18.

Watu hao sita wanaidwa kuteswa, kunyanyaswa,  kushinikizwa kukiri makosa , kukataliwa msaada wa kisheria wakati wa kesi na hawakuwahi kupewa fursa ya mfumo wa kutoa malalamiko yao.

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wamesema “Hukumu ya kifo na unyongaji kwa makosa yaliyotendwa na watu waliokuwa na umri wa chini ya miaka 18 wakati wa tukio , inakwenda kinyume na viwango vya sheria za kimataifa” na kuongeza kuwa “ Kama nchi mwanachama wa mkataba wa haki za mtoto , Saudi Arabia inawajibika kumchukukulia kila mtu aliye na umri wa chini ya miaka 18 kuwa ni mtoto na watoto hawapaswi asilani kupewa hukumu ya kifo, kwahi hilo linakiuka mila na desturi za sheria za kimataifa na kufanya adhabu hiyo kuwa ni utesaji. Na katika mazingira haya kuwanyonga watu hawa sita itakuwa ni mauaji ya kiholela.”

Wataalam hao wamekumbusha kwamba Saudi Arabia hivi karibuni imetathimini sharia yake namba 114 kuhusu barubaru lakini wanasikitika kwani marekebisho yaliyofanywa katika sheria hiyo yameendelea kushindwa kuwalinda watoto. Sheria mpya bado inaruhusu kutolewa kwa hukumu ya kifo dhidi ya watoto wahalifu wa umri wa kati ya miaka 15 na 18.

Wataalam hao wamehimiza kwamba, Saudi Arabia ni lazima ihakikishe kwamba watoto ambao hawajatendewa haki katika kesi zao waachiliwe huru mara moja na wale ambao walikatiwa hukumu ya kifo hukumu zao zibadilishwe kwa mujibu wa viwango vuya kimataifa vya haki kuhusu barubaru na kwa kuzingatia mapendekezo yam waka 2016 ya kamati ya haki za mtoto. Na kuongeza kuwa

“Saudi Arabia lazima irekebishe sharia yake kwa mtazamo wa kutowahukumu kifo watoto.” Hivi sasa wataalam hao wanafanya mawasiliano na serikali ya saudia kuhusiana na kesi hiyo.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter