Idadi kubwa ya wanaosafirishwa kiharamu ni wanawake na wasichana: Mtaalam

26 Oktoba 2018

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linapaswa kuhakikisha kuwa wanawake wanachukua nafasi kubwa ya mchakato wa kujenga amani kama njia ya kuzuia usafirishaji haramu wa watu na kuepusha utumikishaji kabla,wakati na hata baada ya migogoro.

Mtaalam Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya usafirishaji haramu  wa binadamu hususan wanawake na watoto, Bi Maria Grazia Giammarinaro amesema hayo katika ripoti yake kwa Baraza Kuu  la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani.

Amesema kuwa  usafirishaji haramu wa binadamu unapaswa kuchukuliwa kama ukiukwaji wa haki za binadamu badala ya kuwa suala la kiusalama.

Bi. Giammarinaro, amesema kuwa, “ usafirishaji haramu ambao kwa sehemu kubwa unawaathiri wanawake na wasichana, kwa kawaida husababisha shida zingine kama vile mimba zisizohitajika, utoaji mimba wa kulazimishwa, na magonjwa ya  kingono.”

 Ameongeza kuwa “ hatua za kinga kama vile kuwepo kwa makazi, chakula, elimu kwa watoto pamoja na afya ya masuala ya uzazi hayahusishwi katika mikataba pamoja na mipangilio ya amani.”

Mtaalam huyo maalum ameongeza  kuwa kuwajumuisha wanawake zaidi katika hatua za wakati wa mgogoro na hata baada yake kutaleta mwamko kuhusu hali ya hatari waliyo nayo wanawake na wasichana.

Amesema upangaji na utekelezaji wa msaada kwa waathirika wa usafirishaji haramu ukiwa unashirikiana kwa karibu na walionusurika na vilevile  mashirika kuendeleza haki za wanawake ni muhimu mno katika kuzuia usafirishaji na pia unajenga hatua za kuwawezesha wanawake.

Ripoti ya Giammarinaro inataka suala la usafirishaji haramu lijumuishwe kikamilifu katika ajenda za Baraza la Usalama kuhusu   wanawake, amani na usalama ambayo inatoa kipaumbele umuhimu wa kushirikishwa  kwa wanawake  katika mchakato wote wa amani, kuanzia uzuiaji, ujenzi wa amani na pia ulinzi wake.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter