Mtanzania Rebeca Gyumi aibuka kidedea tuzo ya haki za binadamu ya UN

26 Oktoba 2018

Rebeca Gyumi, mwanaharakati wa haki za wanawake na wasichana nchini Tanzania pamoja na watu wengine wawili na shirika moja la kiraia, wameshinda tuzo ya mwaka huu ya haki za binadamu

Washindi hao wametangazwa na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernanda Espinosa ambaye kupitia ukurasa wake wa Twitter amewapongeza kwa mchango wao wa kusongesha mbele haki za binadamu.

Hii ni tuzo ya 10 ambayo mwaka huu inaendana na miaka 70 ya tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ambapo washindi hao watapokea tuzo hizo tarehe 10 mwezi disemba mwaka huu kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Taarifa ya ofisi ya  Kamishna wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa imefafanua kazi za washindi hao akitolea mfano Rebeca Gyumi.

Bi. Gyumim muasisi na mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya Msichana Initiative nchini Tanzania, kwa miaka 8 amekuwa akihoji uhalali wa ibara ya 13 na 17 ya sheria ya ndoa yam waka 1971 nchini Tanzania ambayo inahurusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 na 15 kwa ridhaa ya wazazi au mahakama.

Taarifa hiyo inasema “Bi. Gyumi alishinda kesi hiyo mbele ya Mahakama Kuu ya Tanzaina mwaka 2016.”

Mshindi mwingine ni Asma Jahangir mwanaharakati mwanasheria wa Pakistani ambaye amefariki dunia mwaka  huu.

Marehemu Jahangir kwa miongo mitatu amekuwa akitetea haki za wanawake, wasichana, watoto na makundi madogo ya kidini na maskini nchini mwake ambapo alifungua kituo cha msaada wa sheria. Ingawa hivyo alikuwa akikumbwa na misukosuko lakini alikuwa na uwezo wa kushinda kesi zilizokuwa na utata.

Kwa upande wake, mshindi  mwingine Joênia Wapichana au Joênia Batista de Carvalho, mwanaharakati wa haki za watu wa jamii ya asili nchini Brazil, ni mwanamke wa kwanza wa jamii hiyo kuwa mwanasheria.

“Baada ya kuwasilisha mbele ya tume ya haki za binadamu ya nchi za Amerika, Bi. Wapichana alikuwa mwanasheria wa kwanza wa jamii ya asili kuingia Mahakama Kuu ya Brazil.

Nalo shirika la Front Line Defenders Ireland ambalo linachechemua na kulinda haki za binadamu nchini Ireland linahusika na kulinda mahitaji ya watetezi ili waweze kuendelea na kazi zao bila hatari, vitisho wala kukamatwa.

Tuzo ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa hutolewa kwa watu binafsi na mashirika kwa kutambua mchango wao wa kipekee katika kuendeleza na kulinda  haki za binadamu na uhuru wa msingi wa binadamu kwa mujibu wa tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilianzisha tuzo hii kwa azimio la tarehe 10 disemba 1968 wakati tamko la haki za binadamu lilipotimiza miaka 20 tangu kupitishwa.

Tuzo imetolewa mwaka 1973, 1978, 1988, 1993, 1998, 2003, 2008 na 2013.

Kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, “tuzo hii ni fursa ya siyo tu ya kutambua mchango wa umma katika kusongesha haki za binadamu bali pia kutuma ujumbe dhahiri kwa watetezi wa haki za binadamu duniani kote kuwa jamii ya kimataifa inashukuru na inaunga mkono juhudi zao za kila siku za kusongesha  haki za binadamuu.

Watu wengine waliowahi kushinda tuzo hii ni Eleanor Roosevelt, Martin Luther King, Nelson Mandela, Jimmy Carter, Denis Mukwege, Malala Yusafzai, Shirika la kutetea haki za wafungwa, Amnesty International na kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu, ICRC.

Mwezi septemba mwaka 2016 Rebecca alishinda tuzo ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kwa mchango wake wa kukomesha ndoa za utotoni nchini Tanzania.

 

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter