Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bado tunatafiti iwapo chanjo dhidi ya Ebola ina madhara au la kwa wajawazito- WHO

Chanjo ya HPV hupatiwa kwa wasichana ili kuepusha saratani ya kizazi. Pichani ni nchini Brazil msichana akipatiwa chanjo hiyo ambayo hutolewa kwa wanafunzi wa shule za umma na binafsi
PAHO/WHO
Chanjo ya HPV hupatiwa kwa wasichana ili kuepusha saratani ya kizazi. Pichani ni nchini Brazil msichana akipatiwa chanjo hiyo ambayo hutolewa kwa wanafunzi wa shule za umma na binafsi

Bado tunatafiti iwapo chanjo dhidi ya Ebola ina madhara au la kwa wajawazito- WHO

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema bado linatafiti iwapo chanjo dhidi ya Ebola ina madhara yoyote ya kiafya dhidi ya wanawake wajawazito.

Mwenyekiti wa jopo la ushauri wa kimkakati kwa WHO kuhusu masuala ya chanjo, SAGE, Dkt. Alejandro Cravioto amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, kufuatia kikao cha siku mbili cha jopo hilo.

Dkt. Cravioto amesema, “kwa hiyo kile ambacho tunataka kubaini kwa upande mmoja ni athari gani anapata mwanamke ambaye hajapatiwa chanjo kwenye mazingira ya sasa ambapo wengine wamepatiwa chanjo kwenye mzunguko wa utoaji wa chanjo dhidi ya Ebola huko Afrika Magharibi na sasa Jamhuir ya Kidemokrasia ya Congo. Ushahidi tulio nao ni kwamba hata kama wanawake hawajapatiwa chanjo kwenye makundi ya awali, bado wanaonekana hawambukizwi, jambo ambalo ni dalili nzuri. Tuna matumaini kuwa katika miezi michache ijayo tutakuwa na taarifa zaidi kutoka kwenye uchambuzi wa kina wa wanawake ambao walipatiwa chanjo ilhali ni wajawazito, na ndipo tutafahamu iwapo chanjo hiyo ni salama kwa wajawazito au la.”

Utoaji chanjo ya Ebola
WHO/S. Hawkey
Utoaji chanjo ya Ebola

Hata hivyo Dkt. Cravioto amesema mwisho wa siku itakuwa ni juu ya mjamzito mwenyewe baada ya kupatiwa taarifa zote kuhusu chanjo hiyo, kuamua iwapo anataka kupatiwa hiyo chanjo au la na kwamba hadi hivi sasa  hakuna hitimisho iwapo ina madhara au la.

Jopo hilo pia lilijadili chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, Human Papiloma Virus, HPV ambayo hupatiwa watoto wa kike.

Dkt. Cravioto akaulizwa na waandishi wa habari ni maamuzi yapi waliyofikia katika kuondoa shida ya upatikanaji wa chanjo hiyo na jibu ni kwamba tuna kikwazo cha upatikanaji ambacho tunapaswa kushughulikia. Hakuna chanjo za kutosha. Watengenezaji wote wawili wa chanjo hii walikuwepo kwenye mkutano na wote wamekubali kusaidia kuharakisha kupata suluhisho ya tatizo hili, Wote wako tayari kuchagiza uzalishaji wa chanjo ili  katika siku zijazo tuwe na chanjo za kutosha kwa ajili ya kutumika kwenye nchi zote ambazo zimeanza au zinataka kuanza kutoa chanjo hasa kwa wasichana, ili hatimaye tufanikiwe lengo letu la kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake.”

SAGE ni jopo lililopo chini ya WHO na hutoa ushauri kuhusu aina zote za chanjo zinazotolewa kwa mwongozo wa shirika hilo la afya ulimwenguni.