Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yatumia hawala ya fedha kuimarisha usaidizi Yemen

Msaada wa fedha taslimu huko Yemen unasaidia familia kupata  huduma muhimu za kijamii.
UNICEF/Yemen
Msaada wa fedha taslimu huko Yemen unasaidia familia kupata huduma muhimu za kijamii.

UNHCR yatumia hawala ya fedha kuimarisha usaidizi Yemen

Msaada wa Kibinadamu

Kutokana na kuzidi kudorora kwa hali ya kibinadamu nchini Yemen, huku fursa za kufikisha misaada ya kibinadamu kwa wahitaji zikiwa ni finyu, Umoja wa Mataifa umewekea msisitizo mpango wake wa kuwapatia fedha wahitaji ili waweze kujipatia mahitaji yao kwa urahisi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema mpango huo wa kufikisha fedha kwa wahitaji kwa njia ya hawala ya fedha umekuwa ndio muarobaini kwa kuwa nchini humo watu watatu kati ya wanne wanategemea misaada.

Msemaji wa UNHCR huko Geneva, Uswisi, Andrej Mahecic  amesema “fedha hizo zinapatiwa kaya baada ya upembuzi wa kina unaofanywa na wadau wa UNHCR nchini kote, na mara nyingi kwenye maeneo ambayo ni magumu kufikika. Familia ambazo zinachaguliwa kupata fedha hizo kukimu mahitaji yao kama vile ya afya au pango la nyumba hupokea fedha kwa mfumo wa hawala.”

Amesema hivi sasa wanashirikiana na benki ya Al-Amal kusambaza fedha hizo moja kwa moja kupitia mfumo huo ambao unategemewa sana Yemen licha ya mapigano yanayoendelea.

“Baada ya upembuzi wa kina, mnufaika anapokea ujumbe mfupi kwenye simu yake na fedha hiyo anaweza kuipata kwenye mawakala wa benki hiyo waliosambaa nchini kote.”

Mwezi huu wa Oktoba pekee, UNHCR imefikia zaidi ya familia 22,000 ikiwa ni jumla ya watu 150,000 walioko majimbo 14 ambayo yamegubikwa zaidi na vita.

Bwana Mahecic amesema msaada kupitia fedha taslimu ndio njia bora zaidi na fanisi ili kuendeleza utu wa wananchi wa Yemen.

Hadi sasa UNHCR imetoa jumla ya dola milioni 33 kama fedha taslimu kwa wahusika na lengo ni kufikisha jumla ya dola milioni 41 kabla ya mwisho wa mwaka huu.