Wauza silaha fuateni taratibu muepushe mapigano Afrika

26 Oktoba 2018

Hivi karibuni katika mlolongo wa mijadala ya Afrika kwenye makao makuu ya Umoja wa  Mataifa kulifanyika mkutano wa siku moja kuhusu jinsi jamii ya kimataifa inaweza kukomesha milio ya bunduki barani Afrika, mkutano ambao ulihudhuriwa na wawakilishi wa nchi wanachama wakiwemo wabunge.

Mizozo na vita vikiendelea kugubika bara la Afrika, bunge la Kenya limetaja miongoni mwa hatua muhimu za kuondokana na mapigano hayo  yanayokwamisha harakati za bara hilo kusonga mbele.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na mambo ya nje ya Bunge la Kenya, Richard Tong’i ametaja mambo hayo akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili  ya Umoja wa Mataifa baada ya kushiriki mkutano jijini New York, Marekani wenye lengo la kukomesha mapigano Afrika.

Amesema "hizi silaha hazitoki kwetu. Sisi hatutengenezi silaha. Nyingi zinatoka nchi za Ulaya na tumewauliza pia watusaidie kwa njia moja kuhakikisha wanapatia silaha kwa serikali iliyoko madarakani, si kwa kila mtu akienda kwa njia ya mkato anaweza kununua silaha. Lakini sisi nasi iwapo tukikosana au  mtu akishindwa kura au anasema ameibiwa kura na hizi nchi za Ulaya zinaingilia na kumpatia silaha."

 

Bwana Tong’i akanukuu usemi ya kwamba amani kwa jirani  yako ndio amani kwako jambo ambalo anasema, “kama jirani hana amani, nawe hutakuwa na amani. Kama waafrika haina amani, hata wazungu nao watakuwa hawana amani. Kama tunataka kupigana na  ugaidi lazima tuhakikishe pia kuna amani Afrika. Tuhakikishe pia watoto wa Afrika wana chakula, na vijana nao wana kazi. Kama mtu ana mpangilio wa kuishi vizuri kesho, huyu mtu ni rahisi sana kumuelezea kuhusu matatizo ya kuwa na silaha zisizo halali.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud