Ujumuishaji wanawake kwenye amani usifanane na ‘kupakana mafuta kwa mgongo wa chupa’- Phumzile

25 Oktoba 2018

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN-Women, Phumzile Mlambo-Ngucka ametaka jamii ya kimataifa iachane na harakati za juujuu zisizoweza kuleta matunda katika kujumuisha wanawake kwenye ulinzi na amani duniani.

Bi. Mlambo-Ngcuka amesema hayo leo mjini New York, Marekani wakati akiwasilisha mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ripoti ya mwaka huu Katibu Mkuu kuhusu utekelezaji wa ajenda ya uwezeshaji wanawake kiuchumi na kisiasa kama mbinu ya kupata amani na usalama duniani.

Mkuu huyo wa UN-Women amesema wito wake huo unazingatia ukweli kwamba, “mwaka mmoja uliopita kwenye ukumbi huu huu, nilielezea hofu yangu juu ya takwimu zitokanazo na viashiria vilivyofuatiliwa kwenye michakato ya amani na usuluhishi. Michakato yote kama siyo kukwama imeachwa. Na kwa sababu hiyo ripoti yetu ya mwaka huu inajikita katika michango yenye maana ya wanawake kwenye amani.”

Akifafanua ametolea mfano kile ambacho wamebaini baada ya kuchanganua takwimu kwa misingi ya kijinsia akisema, “ni mikataba 3 tu ya amani kati ya 11 iliyotiwa saini mwaka 2017 ilikuwa na vipengele kuhusu usawa wa kijinsia na hivyo kuendeleza hofu ya mwaka uliotangulia kuhusu mwelekeo wa kutia shaka. Katika mikataba 1500 iliyotiwa saini kati yam waka 2000 hadi 2016, ni 25 tu ndio iliibua dhima ya ushiriki wa wanawake kwenye awamu ya utekelezaji.”

Amesema pamoja na changamoto ni lazima kuangazia fursa na kuwa na matumaini akitaja vipaumbele vitatu ikiwa ni pamoja na kupigia chepuo michakato ya amani inayojumuisha wanawake, kuongeza kiwango cha uchangiaji kwenye mfuko wa UN wa ujenzi wa amani na tatu kuchukua kila hatua kulinda wanawake watetezi wa haki za binadamu na wajenzi wa amani kwenye eneo ya mizozo.

Bi. Randa Siniora Atallah, Mkurugenzi Mkuu wa kituo cha msaada wa sheria kwa wanawake akihutubia Baraza la Usalama kuhusu wanawake, amani na usalama
UN /Manuel Elias
Bi. Randa Siniora Atallah, Mkurugenzi Mkuu wa kituo cha msaada wa sheria kwa wanawake akihutubia Baraza la Usalama kuhusu wanawake, amani na usalama

Bi. Mlambo-Ngcuka amewaeleza wajumbe kuwa “mabadiliko yako mikononi mwetu. Matukio ya sasa yanaweza kutwamisha matumaini yetu na kuvunja nia yetu. Maendeleo yetu yanaweza kuwa ya kusuasua yakikumbana na vikwazo lakini naamini haikataliki. Iwapo wanawake wataungwa mkono ili wajipange vyema, nalo hili halizuiliki.”

Mjadala ulikuwa ni wa wazi ukileta wawakilishi wa mashirika ya kiraia akiwemo Randa Siniora Atallah.

Bi. Attallah ambaye ni Mkurugenzi wa kituo cha msaada wa sheria kwa wanawake  wa kipalestina amewaeleza wajumbe wa Baraza kuwa kitendo cha kupunguzwa kwa bajeti ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wapalestina, UNRWA, kimekuwa na madhara makubwa kwa wanawake wa kipalestina, hususan kiafya na kielimu.

“Uharibifu wa miundombinu umekuwa na madhara makubwa kwa familia na maisha ya wanawake na wasichana kwa kuwa wanashindwa kupata maji, chakula, huduma za kujisafi, umeme na afya,” amesema Bi. Atallah.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter