Vitisho vya Burundi dhidi ya tume ya uchunguzi ya UN havistahili na vifutwe:Bachelet

25 Oktoba 2018

"Taarifa ya jana ya Balozi wa Burundi kwenye Umoja wa Mataifa Albert Shingiro kushambulia ripoti ya tume huru ya kimataifa ya Uchunguzi iliyoanzishwa na Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa inasikitisha na kwa mada na sauti iliyotumika."

Hayo yamesemwa leo na kamishna mkuu wa haki za binadamu Michelle Bachelet akiongeza kuwa vitisho vya kuwashitaji wajumbe wa tume hiyo ya uchunguzi wa ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Burundi kutokana na kazi yao waliyoifanya kwa ombi la baraza la haki za binadamu ambalo ni chombo cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, havikubaliki na lazima Burundi itengue kauli hiyo mara moja.

Ameongeza kuwa mashambulizi binafsi yaliyotolewa na balozi Shingiro kwenye kikao cha kamati ya tatu ya Umoja wa Mataifa dhidi ya mwenyekiti wa tume ya uchunguzi Doudou Diène kwa kumlinganisha na mshiriki wa biashara ya utumwa yalikuwa ni ya fedheha na ya  udhalilishaji.

Hivi sasa tume hiyo ya uchunguzi imeongezewa muda wa mwaka mmoja zaidi. Akizungumza katika mahojiano maalumu na UN News kuhusu matarajio ya tume hiyo baada ya kuongezewa muda mwenyekiti huyo Doudou Diène amesema

(SAUTI YA DOUDOU DIENE)

“Kitu cha kwanza tunachokitarajia kwa ujumla ni kusitishwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu na kuheshimu haki za binadamu.Hiki ndicho kiini cha jukumu letu. Wajibu wetu ni kuorodhesha ukiukwaji wa haki za binadamu na hivyo kukomesha ukiukwaji wa haki za binadamu. Tumaini letu la pili ni kwamba ripoti yetu iweze kusaidia watu wa Burundi, taasisi za nchi hii, ili kubadilika kuelekea hali ya demokrasia inayoheshimu haki za binadamu na misingi ya sheria, uhuru wa habari na kujieleza. Na mwisho , tunatumai kwamba watu wote walioathirika na mgogoro wa Burundi ni lazima wakumbukwe kutoka mbali. Ni kanda ambayo imeunganishwa na historia ya kikoloni, ambapo utamaduni wa vurugu umekita mizizi, maelfu ya watu wamekufa wa kwa muda mrefu. Tunafikiria mateso yanayowasibu watu wa Burundi na kile tunachotaka kufanya ni kuchangia kuyaondoa, kukomesha mateso haya na kuwa na katiba ya jamii ya kidemokrasia inayoheshimu haki za binadamu.”

Kamishna mkuu wa haki za binadamu amesema Burundi kama nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa inapaswa kuonyesha heshima kwa taasisi zake na vyombo vyake vingine, sharia na mikakati inayoanzishwa na Umoja huo.

Amesema dharau ya Burundi na majibu ya kupaka matope  matokeo ya uchunguzi wa tume hiyo na kutoiunga mkono kwa madai kwamba ni kibaraka wa shinikizo kutoka nje , lakini pia serikali ya nchi hiyo kushindwa kushughulikia yaliyobainiwa na tume hiyo ni kutowajibika na ni makosa.

Bi. Bachelet ameitaka serikali ya Burundi kutoa taarifa mara moja kutengua kauli yake na kuomba radhi kwa Bwana Diène na wajumbe wengine wa tume, pamoja na Baraza la Haki za binadamu ambalo liliunda tume hiyo ya uchunguzi lakini pia Rais wa baraza hilo aliyeteua wajumbe hao watatu wa tume huru ya uchunguzi kuhusu Burundi.

Burundi hivi sasa ni miongoni mwa nchi wanachama 47 wanaoketi kwenye Baraza la Haki za Binadamu.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud