Kiwango cha vifo vya mama wanaojifungua Sudan Kusini kiko juu : UNFPA
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu la UNFPA limetoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kukabiliana na tatizo la ghasia zilizo na uhusiano wa kingono pamoja na kijinsia nchini Sudan Kusini.
Wito huo umetolewa mjini Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini , na mkunga wa UNFPA nchini humo, Bi Judith Draleru, katika mahojiano na Radio Miraya, Radio ya Umoja wa Mataifa katika taifa hilo.Akisisitiza haja ya kuwapa matumaini waathirika wa ubakaji ambao baadhi hupoteza maisha wakati wa kujifungua mimba ambazo hawakutarajia na pia kugusia hali ilivyo nchini Sudan Kusini.
“ Sisi kama UNFPA mpango wetu wa kimkakati ni kuhakikisha kwamba hakuna yeyote anaeachwa nyuma katika kupata taarifana huduma kuhusu afya ya uzazi ikiwa ni pamoja na haki zao.Tunataka kufikia lengo hili katika kile tunachokiita ajenda ya mabadiliko. Kwanza tunalenga kumaliza vifo vya kina mama wakati wa kijifungua na pili ni kukomesha ukatili wa kijinsia pamoja na ndoa za utotoni lakini pia mila nyingine potovu.”
Pia amesema kuwa UNFPA inaendesha mradi wa kuimarisha huduma za ukunga Sudan Kusini ili kuona kwamba hakuna anaeachwa nyuma kulingana na malengo ya maendeleo endelevu.
UNFPA imekuwa ikiwasaidia waathirika wa ghasia za kingono na kijinsia nchini Sudan Kusini.