Azimio jipya lapitishwa kuimarisha huduma za afya ya msingi duniani
Wanachama wa Umoja wa Mataifa leo kwa kauli moja wamepitisha azimio la Astana lenye lengo la kuimarisha afya ya msingi kwa kila mtu duniani.
Azimio hilo limepitishwa huko Astana Kazakhstan ambako wawakilishi wa nchi hizo wanakutana kwa siku mbili ambapo azimio hilo linawekea msisitizo azimio la kihistoria la Alma-Ata la mwaka 1978 ambalo kwalo kwa mara ya kwanza viongozi wa dunia waliazimia kuimarisha afya ya msingi.
Hatua hii ya leo imechukuliwa wakati ambapo takribani nusu ya wakazi wa dunia hawana uwezo wa kupata huduma za afya ya msingi ikiwemo matibabu dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na yale yasiyo ya kuambukiza pamoja na vifo vya wajawazito na watoto wachanga bila kusahau afya ya akili na afya ya uzazi.
Kupitia azimio hilo, nchi wanachama zimeahidi mambo makuu manne, mosi kupitisha maamuzi thabiti ya kisiasa kuhusu sekta ya afya, pili kuweka mifumo endelevu ya afya ya msingi, tatu kujengea uwezo jamii ili ziweze kufikia huduma hizo nan ne kuhamasisha wadau kusaidia sera za kitaifa, mikakati na mipango hiyo.
Taarifa ya shirika la afya ulimwenguni, WHO imesema kupitia azimio la Astana, WHO pamoja na shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF watasaidia serikali na mashirika ya kiraia kulitekeleza sambamba na kuwasihi waunge mkono azimio hilo.
Akizungumzia azimio hilo Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henriette Fore amesema, ijapokuwa dunia hivi sasa inaonekana kuwa ni eneo lenye afya zaidi kwa watoto, kuliko wakati wowote ule, bado watoto wapatao milioni 6 hufariki dunia kila mwaka kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano kutokana na magonjwa yanayozuilika na zaidi ya milioni 150 wamedumaa."
Amesema "sisi jamii ya kimataifa tunaweza kubadilisha mwelekeo huu kwa kuweka huduma bora za afya karibu na jamii ambazo zinahitaji na hii ndio maana ya huduma ya afya ya msingi."
Washiriki wa mkutano huo uliondaliwa na kwa pamoja na WHO, UNICEF na serikali ya Kazakhstan na ambao unamalizika kesho ni pamoja na mawaziri wa afya, fedha, elimu, ustawi wa jamii na wachechemuzi wa afya bila kusahau vijana na wanaharakati.